Sidhani kama Simba wana kitu kikubwa cha kupoteza katika hili. Kuna kocha huwa anawaweka katika wakati mgumu akiamua kuondoka zake. Kuna aina ya mpira anaweza kuondoka nayo. Hadi sasa hatutajua mpira wa Fadlu ni upi hasa. Kuanzia pale alipoishika timu na mpaka pale alipokwenda likizo kisha akarudi, akahusika katika usajili na kisha kwenda na timu kambini Misri.
Wakati ikiwa pale Ismailia chini ya Fadlu sidhani kama Simba imetengeneza aina yoyote ya mpira wa kushtua chini ya Fadlu. Siku hizi makocha wanatengeneza falsafa zao. Unaweza kuchagua kuwa bora katika kushambulia, au kukaa na mpira, au kujihami. Sijaona LOLOTE ambalo Fadlu amelitengeneza kwa ufasaha wakati timu ikiwa kambini kule Misri.
Tukianzia mechi ya Gor Mahia katika siku ya Simba Day. Wageni waliwafundisha wenyeji namna ya kukaa na mpira kwa muda mrefu. Bahati mbaya tu wageni waliruhusu mabao mawili. Halafu likaja pambano la Simba na Yanga. Simba walionekana kucheza vizuri. Sio kwamba walikuwa wazuri, hapana, ni vile tu Yanga walitarajiwa kuwa wazuri zaidi ya Simba lakini hawakucheza katika kiwango chao. Bado mwisho wa yote Fadlu aliendelea kuweka rekodi ya kupoteza pambano jingine la Dabi dhidi ya mtani kitu ambacho kimekuwa cha kawaida kwake.
Na Jumamosi jioni Simba ilikuwa Gaborone ikicheza pambano la kimataifa la ushindani dhidi ya Gaborone United Simba haikuonyesha kama ilikuwa kambini Misri ikipika kitu. Ilicheza ovyo ingawa ilishinda 1-0. Sijakutana na shabiki wa Simba aliyeridhika na kiwango cha timu
Kama akiondoka sasa Simba watakuwa katika nafasi nzuri ya kuanza na kocha mpya kabla msimu haujachanganya. Labda wachezaji watamuelewa mapema kocha mpya wakati msimu angali ukiwa mchanga.”
— Legend, Edo Kumwembe. [JichoLaMwewe]