LIVERPOOL: MENEJA wa Liverpool, Arne Slot amekerwa na kadi nyekundu aliyopewa mshambuliaji wake Hugo Ekitike baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Southampton kwenye mchezo wa Kombe la FA usiku wa Jumanne kisha kuvua jezi wakati wa kushangilia.
Mfaransa huyo, ambaye alichukua nafasi ya mfungaji wa bao la kwanza Alexander Isak, alipata kadi ya kwanza ya njano baada ya kuupiga mpira nje kwa hasira na ya pili baada ya kufunga bao la pili dakika tano kabla ya mchezo kumalizika na kuwaacha Liverpool wakilinda ushindi wa mabao 2-1 wakiwa 10.
“Nadhani ni ujinga pia hata kama huna kadi ya njano. Labda mimi ni wa kizamani kidogo, nilifunga mabao pia labda sio katika daraja hili. na ikiwa labda ningewapiga chenga wachezaji wawili watatu, jambo ambalo sikuwahi kufanya, na kisha nikafunga kwenye kona ya juu, basi labda unaweza kusema ‘oh, sasa ni muda wangu’”
“Lakini kama ningefunga bao sawa na alivyofunga ningegeuka na kumwendea Federico Chiesa na kusema ‘Yote ni sababu yako, Federico. Assist nzuri, run nzuri na nisingelazimika kufanya mambo mengi’.
“Ulikuwa ujinga wa hali ya juu, (Ekitike) amefanya jambo la kipuuzi sana sasa amesimamishwa na tuna kazi kubwa Jumamosi hilo ni jambo lisiloifaa klabu wala yeye mwenyewe.” – Slot ameiambia Sky Sports
Baadaye Ekitike aliomba radhi kwenye ukurasa wake wa Instagram akisema alishindwa kuzuia hisia zake baada ya kupata bao hilo. Vinara wa ligi Liverpool, wakiwa na rekodi ya ushindi wa 100% msimu huu, wana safari ngumu ya ugenini dhidi Crystal Palace ambayo pia haijapoteza mchezo kwenye ligi.
The post Kadi nyekundu ya Ekitike yamkera Slot first appeared on SpotiLEO.