DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Azam FC Florent Ibenge amesema bado hajatosheka na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Katika mchezo huo wa ufunguzi kwao, Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 mabao yakiwekwa kimiani na Nassoro Saadun na Feisal Salum.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Ibenge alisema ushindi huo ni jambo la faraja, lakini bado kuna mambo mengi ya kuboresha ili timu iwe imara zaidi katika mechi zijazo.
“Nadhani mchezo wa leo haukuwa mbaya kutazama. Ninafuraha kwa sababu ukiangalia takwimu za wachezaji wangu, wamekimbia sana na kuunda nafasi nyingi za kufunga. Lakini mpinzani wetu alikuwa na nafasi moja pekee. Hilo linanipa furaha kwa kuwa napenda timu yangu kusonga mbele na kuweka msimamo,” alisema Ibenge.
Hata hivyo, kocha huyo aliongeza kuwa pamoja na ushindi huo, hawezi kuridhika kwa sababu anataka kuona kikosi chake kikiendelea kuboresha kiwango chao kila mara.
“Tunafanya kazi kila siku kwenye mafunzo, kwa hiyo wanapaswa kuendelea kuboresha. Sijaridhika kabisa, na kutoridhika huko ndiko kunatufanya tuendelee kufanya kazi kwa bidii zaidi,” aliongeza.
The post “Bado sijatosheka” – Ibenge: first appeared on SpotiLEO.