MUNICH: MABINGWA wa Bundesliga Bayern Munich wanatamani muendelezo kwenye mwanzo mzuri wa mabao nane wa Harry Kane katika mechi nne za kwanza za Bundesliga dhidi ya wageni wao Werder Bremen kesho Ijumaa huku kukiwa na uvumi unaoongezeka juu ya uwezekano wa nahodha huyo wa England kurejea EPL.
Kane alifunga hat-trick, zikiwemo penalti mbili, katika ushindi wao wa 4-1 dhidi ya Hoffenheim wiki iliyopita huku pia akiwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Bundesliga kufunga mfululizo penalti 17.
Kwa msaada mkubwa wa uwezo wa Kane wa kupachika mabao, Bayern sasa wameweka rekodi ya mwanzo mzuri zaidi wa msimu kwa kufunga magoli 18 katika mechi zao nne za kwanza za ligi hiyo ikiwa timu ya kwanza kufanya hivyo kwenye historia ya Bundesliga.
“Siku zote amekuwa mfungaji mzuri lakini nadhani amefanya uamuzi wa kujua jinsi ya kutengeneza mabao hayo kwa ufanisi. Kane ni kiongozi mzuri kwenye timu yetu na ni mmoja wa wachezaji wanaofanya vizuri, hilo ni jambo linalofanya nijione nina bahati sana kama kocha.”- kocha wa Bayern Vincent Kompany aliwaambia wanahabari
Bayern wanauhitaji sana umakini wa Kane kwenye mchezo wa Werder Bremen kabla ya msururu wa mechi ngumu za Bundesliga, wakianza na Eintracht Frankfurt wikiendi ijayo kisha kukiwasha na Borussia Dortmund nyumbani.
The Bavarians, ambao watasafiri pia kuifuata Pafos ya Cyprus kwenye mchezo unaofuata wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne, wako juu ya msimamo wa Bundesliga na pointi 12.
The post Bayern yamtwisha zigo Harry Kane first appeared on SpotiLEO.