Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi wa Mchinga katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi kwa CCM, mkoani Lindi tarehe 25 Septemba, 2025.
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga Salma Kikwete mara baada ya kuhutubia wananchi wa Jimbo hilo mkoani Lindi tarehe 25 Septemba, 2025.
………..
NA JOHN BUKUKU- MCHINGA, LINDI
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Jimbo la Mchinga kuwa serikali yake itaendelea kutoa ruzuku na huduma mbalimbali ili kuinua sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi. Ameyasema hayo Septemba 25, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Chama hicho mkoani Lindi.
Dkt. Samia amesema serikali itaendelea kuchimba visima na kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Aidha, amesisitiza kuwa ruzuku za pembejeo, dawa za kuua wadudu na dawa za magonjwa ya mikorosho zitaendelea kutolewa ili kuongeza tija kwa wakulima.
Amebainisha pia kuwa serikali itaendelea kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umeleta manufaa makubwa kwa wakulima wa korosho. Aidha, amesema vyama vya ushirika vimeimarishwa na sasa vina mchango mkubwa katika maendeleo ya wakulima na hata katika kampeni za chama hicho.
Katika sekta ya umwagiliaji, Dkt. Samia amesema serikali imetenga shilingi bilioni 30.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi katika Bonde la Kinyope, Rutamba na Kilangala ili wakulima waweze kuzalisha mara mbili kwa mwaka. Ameongeza kuwa mazao ya chakula yamekuwa pia mazao ya biashara yanayouzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Vilevile, amesema serikali itajenga soko kubwa la mazao ya mbogamboga na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ili wakulima wanufaike zaidi. Amebainisha kuwa ruzuku ya chanjo kwa mifugo itaendelea kutolewa, ambapo serikali italipia nusu ya gharama huku chanjo za kuku zikitolewa bure.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha mifugo ya Tanzania inakidhi viwango vya kimataifa ili nyama na mazao mengine ya mifugo yaweze kuuzwa nje ya nchi. Aidha, amesema serikali inaendelea kujenga majosho na machinjio bora.
Kuhusu sekta ya uvuvi, Dkt. Samia amesema serikali imetoa mikopo ya boti za kisasa yenye thamani ya shilingi milioni 712, na kwamba katika awamu ijayo vifaa zaidi vitatolewa ili kuendeleza sekta hiyo.
Kwa upande wa afya, amesema serikali imeimarisha huduma za rufaa mkoani Lindi, na kwamba wagonjwa wa magonjwa makubwa pekee ndio watakaohamishiwa Muhimbili au hospitali nyingine. Aidha, amesema serikali itaendelea kuajiri watumishi wa afya wapya 500 ambapo mkoa huo utapewa kipaumbele.
Katika elimu, Dkt. Samia ameeleza kuwa serikali inaendelea kujenga shule za msingi na sekondari pamoja na nyumba za walimu. Aidha, amesema Mchinga imechaguliwa kuwa na shule maalum ya mchepuo wa sayansi kwa wasichana, huku ujenzi wa Shule ya Amali ya Jakaya Kikwete ukiwa umefikia asilimia 70.
Kuhusu sekta ya nishati, Dkt. Samia amesema vijiji na vitongoji vyote vitapatiwa umeme, na serikali inaendelea kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza matumizi ya kuni na kulinda mazingira.
Aidha, amesema mgao wa asilimia 10 kwa makundi maalum utaendelea kutolewa kwa kuzingatia makusanyo ya halmashauri. Amewataka wananchi wa Mchinga kuongeza uzalishaji na kulipa kodi ili kuongeza mapato ya ndani.
Pia, kuhusu miundombinu, Dkt. Samia amesema serikali itaendelea kuboresha barabara zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ikiwemo barabara ya Milola hadi Kiwawa pamoja na nyingine zilizoorodheshwa.