NA JOHN BUKUKU- LINDI
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imeendelea na mazungumzo ya kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa gesi asilia ya kimiminika (LNG) unaotarajiwa kujengwa mkoani Lindi.
Ameyasema hayo Septemba 25, 2025, katika muendelezo wa kampeni za chama hicho wakati akizungumza na wananchi na wakazi wa Mkoa wa Lindi katika uwanja wa Ilulu.
Dkt. Samia amesema mradi huo ni wa kimkakati na utagharimu dola za Marekani bilioni 40, hivyo wawekezaji wanapaswa kuwa na uhakika wa masilahi yao, huku Tanzania nayo ikihakikisha inanufaika ipasavyo na rasilimali hiyo.
“Nataka kuwaambia wana Lindi, mradi huu upo. Tumekuwa na mazungumzo kwa miaka miwili sasa na tupo hatua za mwisho za kukubaliana. Tutakapomaliza kusaini mkataba, pilika za mradi huu zitaanza mara moja,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, amebainisha kuwa mradi wa gesi utakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa na kufungua fursa za ajira kwa vijana. Amesema tayari serikali imeanza ujenzi wa Chuo cha Nishati na Umeme Lindi ambacho kitawapa vijana maarifa na stadi zitakazowawezesha kushiriki moja kwa moja katika shughuli za mradi huo.
“Kile chuo kinaendelea kujengwa ili kuwafundisha vijana wetu na wapate ajira kwenye hilo eneo. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wa Lindi na Watanzania kwa ujumla wananufaika moja kwa moja na gesi asilia,” amesema.
Dkt. Samia amesema mbali na gesi, serikali pia inaendelea kuboresha sekta nyingine muhimu za kijamii na kiuchumi ikiwemo elimu, afya, maji, miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege ili kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji na ustawi wa wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa kufungua ukanda wa kusini, hususan Lindi, Mtwara na Ruvuma, ambao umebarikiwa kwa rasilimali nyingi ikiwemo gesi, kilimo, uvuvi na madini.
Katika sekta ya maji, Dkt. Samia amesema serikali imefikia zaidi ya asilimia 87 ya upatikanaji wa maji safi na salama nchini, na katika awamu ijayo lengo ni kumaliza changamoto hiyo kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hiyo karibu.
Aidha, amebainisha kuwa usambazaji wa umeme umekamilika kwenye vijiji vyote na sasa serikali inalenga kumaliza vitongoji vilivyosalia.
Katika sekta ya usafirishaji, Dkt. Samia amesema serikali imewekeza kwenye barabara, madaraja, bandari na viwanja vya ndege ili kufungua ukanda wa kusini. Amefafanua kuwa barabara kuu ikiwemo Dar es Salaam–Kibiti–Lindi–Mingoyo na barabara ya Mnivata–Newala–Masasi zimetengewa kipaumbele kukamilishwa.
Amesema pia serikali itajenga Uwanja wa Ndege wa Lindi na viwanja vingine vidogo, huku bandari ya uvuvi Kilwa yenye thamani ya shilingi bilioni 279.5 ikiendelea kujengwa.
Aidha, katika sekta ya elimu, Dkt. Samia amesema serikali imejenga vyuo vya VETA karibu kila wilaya na Lindi itanufaika na vyuo vikubwa vitatu ikiwemo Ndaki ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na chuo cha nishati na umeme.
Pia, amebainisha kuwepo kwa shule ya wasichana ya sayansi wilayani Mchinga ambayo itahudumia wanafunzi wa mkoa mzima. Ameongeza kuwa serikali itaendelea kujenga zahanati, vituo vya afya na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Dkt. Samia amesema serikali itaendelea kutoa ruzuku za pembejeo, mbolea, sumu na dawa ili kuongeza tija ya kilimo.
Aidha, ameahidi kuongeza matrekta na zana za kisasa pamoja na kuanzisha vituo vya kukodisha zana za kilimo mkoani Lindi. Amesema “viwanda vya kubangua korosho na kuchakata mafuta vitafufuliwa, na vyama vya ushirika vitapewa nguvu kupitia Benki ya Ushirika yenye mtaji wa shilingi bilioni 55.”
Aidha, Dkt. Samia amesema serikali imenunua boti za kisasa na vifaa vya uvuvi ili kuwawezesha wavuvi, huku ikilenga kujenga viwanda vya kuchakata samaki mkoani humo.
Katika sekta ya madini, amebainisha kuwa Lindi tayari lina soko moja la madini na jingine linajengwa ili kurahisisha biashara ya wachimbaji wadogo, huku serikali ikipanga kuongeza maeneo ya upimaji wa madini nchini.
Pia, Dkt. Samia amesema serikali imeanzisha mfuko maalum wa TAMISEMI wa kusaidia ujenzi wa masoko na stendi kwa halmashauri, ambapo fedha zitakopwa na kurejeshwa kupitia mapato yatakayokusanywa.
Aidha, Dkt. Samia amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa unalenga kufungua rasmi ukanda wa kusini, hususan mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, na kuifanya kuwa kitovu cha uwekezaji na maendeleo ya taifa.