NA MWANDISHI WETU
MSIMU
wa Nne wa Kampeni ya fungua Akaunti, Weka Akiba na Ushinde
inayoendeshwa na Benki ya NMB ‘NMB Bonge la Mpango,’ umezinduliwa Dar es
Salaam leo, na kwa wiki 12 wateja wa benki hiyo watajishindia mamilioni
ya pesa na bidhaa mbalimbali kila wiki, huku mshindi wa jumla
akitarajiwa kujizolea Sh. Mil. 100.
Licha
ya kuhamasisha wateja wa NMB kuendelea kuweka fedha na akiba kwenye
akaunti zao kwa dharura mbalimbali na ustawi wa maisha ya baadaye, NMB
Bonge la Mpango ni sehemu ya mpango mkakati wa kuongeza idadi ya
Watanzania wanaotumia Huduma Jumuishi za Kifedha.
Kampeni
ya NMB Bonge la Mpango ilianza mwaka 2021, kabla ya mwaka uliofuata
(2022) kurejea tena kwa kampeni hiyo ikitumia kaulimbiu ya ‘2merudi
Tena,’ na baadae ya mwaka 2023 kuitwa NMB Bonge la Mpango ‘Moto Ule Ule’
na mwaka huu kuwa NMB Bonge la Mpango ‘Mchongo Nd’o Huu.’
Kampeni
hii imezinduliwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba
Nguvila na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert
Mponzi, mbele ya Mkuu wa Mtandao wa Mauzo na Matawi ya NMB, Doantus
Richard na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio.
Akizungumza
katika uzinduzi huo, Mponzi alisema kampeni hiyo ya miezi mitatu
(Septemba 25 hadi Desemba 19), itahusisha wateja wenye akaunti na wateja
wapya watakaofungua akaunti na kuwa na akiba inayoanzia Sh. 100,000,
ambako droo zitachezeshwa kila wiki, mwezi na fainali.
“Lengo
la kampeni kuongeza idadi ya Watanzania wanatumia huduma za kibenki,
lakini pia kuhamasisha utamaduni chanya wa kujiwekea akiba, ambapo sisi
kama taasisi bora ya kifedha nchini, tunawazawadia wateja wetu
wanaojiwekea akiba zao wenyewe,” alisema Mponzi.
Alibainisha
ya kuwa zawadi kuu ya mshindi wa jumla ni Sh. Mil. 100 itakayotolewa
katika ‘grand finale’ ambayo washindi wengine 6 watajitwalia trekta za
kulimia ‘power tiller’, huku washindi wengine 10 wakijishindia pikipiki
za mizigo ya magurudumu matatu maarufu ‘toyo.’
“Lakini
tutakuwa na washindi wa kila wiki, ambako wateja wetu 10 watajishindia
fedha taslimu Sh. 100,000, huku washindi wengine 9 watajinyakulia kimoja
kati ya Friji, Tv ya kisasa, mashine ya kufulia na jiko la gesi
kulingana na matakwa ya mteja,” alisema Mponzi.
Kwa
upande wa zawadi za droo za kila mwezi, Mponzi alisema benki hiyo
itakuwa ikiwazawadia washindi wanne wa kila mwisho wa mwezi Sh. Mil. 5
kila mmoja, ikiwa na maana wateja wanane katika miezi miwili ya kwanza
watajizolea Sh. Mil. 40 kwa wote.
Naye
Dk. Nguvila, kwa upande wake aliishukuru NMB kwa kuzindulia kampeni
hiyo katika eneo la Kariakoo ambalo ni kitovu cha biashara nchini,
lakini pia kwa namna inavyojitoa katika masuala ya kijamii, ikiwemo
misaada ya vifaatiba na vifaa vya elimu katika hospitali na shule
mbalimbali nchini.
Alisisitiza
kuwa suala la uwekaji wa akiba ni jambo muhimu katika maisha ya kila
siku, ili kumuwezesha mwekaji akiba hususani benki, kumudu kuyakabili
masuala ya dharura, lakini pia kujiepusha na upotevu, wizi na hata
majanga kama ya moto na uharibifu mwingine.
“NMB
ndio benki bora, ndio benki yenye pato kubwa, ndio benki inayotoa gawio
kubwa sana kwa Serikali, lakini zaidi ya yote wanayo Programu ya
Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambayo inasaidia sana utatuzi wa changamoto
katika Sekta za Elimu na Afya,” alibainisha Nguvila.
Katibu
Tawala huyo alishngazwa na ukubwa wa zawadi zilizowekwa na NMB kwa
washindi wa kampeni hiyo, tena kwa kuweka tu akiba itakayomsaidia
mwenyewe, huku akiwataka wafanyabiashara wa Kariakoo, kuchangamkia fursa
hiyo muhimu ili kukua kibiashara na kiuchumi.
Awali,
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK), Martin
Mbwana, aliishukuru NMB kwa kupeleka uzinduzi wa Bonge la Mpango
Kariakoo, eneo ambalo lina kumbukumbu kubwa za udhamini mnono wa benki
hiyo katika Tamasha la Kariakoo Festival 2024.
“Tunaishukuru
sana NMB kwa mambo mengi inayotufanyia, hata ukiangalia ukusaji wao wa
madeni ya mikopo, haitumii nguvu badala yake inatuelimisha na hii maana
yake ni benki inayopenda uhai na ustawi wa wafanyabiashara na biashara
zetu,” alisema Mbwana.