Afisa elimu Takwimu halmashauri ya Arusha idara ya elimu sekondari Meito Laizer ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa halmashauri hiyo akizungumza katika mahafali hayo.
Mkuu wa shule hiyo ,Loishiye Sironga akizungumza katika.mahafali hayo shuleni hapo.
Wahitimu katika.mahafali hayo wakipewa vyeti vyao vya kuhitimu shuleni hapo.
………..
Happy Lazaro, Arusha
IMEELEZWA kuwa kitendo cha wazazi kutochangia chakula mashuleni kwa shule nyingi mkoani Arusha ndio sababu kubwa inayochangia kushuka kwa kiwango cha wanafunzi mashuleni
Aidha hali hiyo imekuwa pia ikisababisha utoro mashuleni kutokana na wanafunzi wengi kutoroka shuleni kwa ajili ya kwenda kutafuta chakula jambo ambalo linachangiwa na wazazi wenyewe.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Afisa elimu Takwimu halmashauri ya Arusha idara ya elimu sekondari Meito Laizer
ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,wakati akizungumza na wazazi pamoja na wanafunzi katika mahafali ya 34 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Oldadai iliyopo kata ya Sokon 2 ambapo jumla ya wanafunzi 184 wamehitimu kidato cha nne shuleni hapo.
“Nimesimamia shule nyingi katika mikoa mbalimbali na huko kote nilipokuwa mwamko wa wazazi ni mkubwa sana katika kusimamia taaluma ya watoto mashuleni kwa maana ya kuchangia chakula ila kwa mkoa wa Arusha swala la wazazi kuchangia chakula limekuwa ni changamoto kubwa sana hali ambayo inachangia pia kiwango cha ufaulu kuendelea kushuka siku hadi siku naombeni sana katika hili kila mzazi aone umuhimu kwani tunakwamisha shule na watoto sisi wenyewe .”amesema.
Aidha amesema kuwa ,kitendo cha wazazi kutochangia chakula mashuleni kinasababisha shule nyingi kutofikia malengo yake kutokana na wanafunzi kushindwa kufanya vizuri ,hivyo amewataka wazazi kushirikiana na shule katika kuchangia chakula mashuleni.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo ,Loishiye Sironga amesema kuwa, shule hiyo ilianza mwaka 1988 na ilijengwa kwa nguvu za wananchi ,serikali pamoja na wadau wengine ambapo ilianza ikowa na wanafunzi 80 na walimu 5 na vyumba vya madarasa 4 .
Sironga amesema kuwa,kiwango cha ufaulu shuleni hapo kimeendelea kupanda mwaka hadi mwaka kwa miaka minne mfululizo na kufuta “F”katika baadhi ya masomo.
“Katika eneo la miundombinu tunaishukuru serikali chini ya Mhe Rais Dokta Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake mwaka 2021 -2022 serikali imefanikiwa kujenga madarasa mapya 5 bweni moja la wasichana na kumalizia madarasa mawili yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi na hatua hiyo imesaidia sana kuondoa msongamano wa wanafunzi madarasani na wanafunzi wa kike kupata nafasi ya kulala hosteli kwa kutumia bweni moja lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80.”amesema Sironga.
Aidha Sironga ametaja changamoto.zinazowakabili shuleni hapo kuwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu hasa madarasa,mwitikio mdogo wa wazazi kutoa chakula.cha watoto wao wawapo shuleni na kupelekea baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu masomo mchana kwa sababu ya njaa,upungufu wa matundu ya vyoo vya wasichana ,ukosefu wa jengo la utawala, kukosekana kwa uzio shuleni,upungufu wa vyumba vya walimu, na kukosekana kwa nyumba ya matroni.
Ameongeza kuwa, lengo ya shule hiyo ni kuongeza ufaulu zaidi kwa kuwa na ufaulu wa daraja 1,2,na tatu na kuondoa kabisa daraja la nne na sifuri,kuongeza mabweni kwa ajili ya “O” level na “A” level.
“Tunaomba kuongezewa kwa mabweni ya wasichana na wavulana kwani wengi wao hawana malezi mazuri huko mtaani na hata nyumbani na hivyo kupelekea wengi kukatisha masomo yao kuendelea kuwa chini,tunaomba pia kuongezewa madarasa pamoja na bweni kwa ajili ya kuanzisha elimu ya kidato cha V na VI(A-level) pamoja na kusaidia ukarabati kwani michango ya wazazi inasuasua.”amesema Sironga .
Naye Mhitimu wa kidato cha nne ,Samsoni Mollel akisoma risala yao amesema kuwa, kwa kipindi wakiwa shuleni hapo wamefanikiwa kitaaluma kwani waliweza kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha pili na wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kidato cha nne pia.
Aidha ametaja changamoto ambazo wameomba zipatiwe ufumbuzi kuwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ya madarasa,upungufu wa mashine za kutolea copy,wazazi wengi kutolipia chakula cha mchana hivyo kulazimu kushinda njaa na kushindwa kufikia malengo yao na ni hatari kwa afya zao pia hivyo wameomba kutatuliwa changamoto hizo ili waweze kufikia malengo yao waliyojiwekea shuleni hapo.