UONGOZI wa Simba SC umebainisha hasara watakazopata kutokana na kuwakosa mashabiki kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, Septemba 28 2025 Uwanja wa Mkapa.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC amesema kuwa walipata adhabu kutokana na makosa ya mashabiki kwenye mechi zilizopita za kimataifa ikiwa ni mchezo wa Al Masry na RS Berkane.
“Hasara ya kwanza tunakosa mashabiki, hasara ya pili tunakosa mapato na hasara ya tatu tunalipa faini ya USD 50,000. Vilevile tumepewa adhabu kutokana na mechi ya fainaili dhidi ya RS Berkane, huku vilevile tuliwasha fireworks. Kwenye mechi ya fainali tumetozwa faini ya USD 35,000. Jumla Tumetoshwa USD 85,000 sawa na Tsh. 200 milioni.
“Tunacheza bila mashabiki kwenye mechi dhidi ya Gaborone United pekee lakini tumefanya makosa mfululizo CAF watakuwa makini na sisi kwelikweli sababu wanaona tunafanya vitendo ambavyo sio vya kiungwana hivyo watakuwa wanaangalia kama Simba Sports SC tumebadilika. Ni lazima tuwe makini kwelikweli ili kuwaonyesha kwamba tumejifunza na tumebadilika. Kuanzia hivi sasa tuchukue taswira mpya kwenye eneo la mashabiki.
“Wapo mashabiki ambao wametaka kuwa sehemu ya maumivu ambayo tunapitia Klabu ya Simba na maumivu yenyewe ni faini ya Tsh. 212,500,000 sawa na USD 85,000. Kwa mapenzi yao mashabiki wameomba kuchangia faini ili kuipunguzia klabu mzigo na sisi tumepokea na tumeridhia mashabiki wachangie hususani kwenye eneo la faini,”.
Leo Simba SC itakuwa na kazi kwenye anga la kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja wa Mkapa, saa 10:00 jioni.Mashabiki watakuwa Coco Beach ambapo hapo wataangalia mpira kwenye Big Screen.