DAR ES SALAAM:WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amemkabidhi hundi ya Sh. Milioni 20 kwa Bingwa wa Dunia wa mbio za Marathon za kilomita 42, Alphonce Felix Simbu, kama zawadi ya kutambua mchango wake mkubwa katika kuipa heshima Tanzania kimataifa.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika juzi, Septemba 27 katika Ukumbi wa Kibo uliopo ndani ya Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wanamichezo na wadau wa michezo nchini.
Zawadi hiyo imetolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa niaba ya Serikali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha na kuthamini mafanikio ya wanamichezo wa Tanzania wanaoiwakilisha nchi kwa mafanikio katika majukwaa ya kimataifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Majaliwa amempongeza Simbu kwa nidhamu, uzalendo na juhudi alizozionesha hadi kufanikisha ushindi huo mkubwa katika mashindano yaliyofanyika jijini Tokyo, Japan.
“Simbu ametufundisha kuwa ushindi huanza na maandalizi, nidhamu na moyo wa kujitolea. Serikali itaendelea kuunga mkono wanamichezo wetu wanaoleta heshima kwa Taifa letu,” amesema Majaliwa.
Kwa upande wake, Simbu ameishukuru serikali kwa kutambua na kuthamini mafanikio yake, huku akiahidi kuendelea kuiwakilisha Tanzania kwa kiwango cha juu zaidi katika mashindano yajayo.
“Hii ni motisha kubwa kwangu na kwa wanamichezo wengine.
“Nashukuru kwa zawadi hii na ninaahidi kuendelea kupambana kwa ajili ya taifa langu,” amesema Simbu kwa furaha.
Aidha, Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Masita ameongeza kuwa zawadi hiyo ni mwanzo tu wa mpango mpana wa serikali wa kuwekeza zaidi katika michezo na kuhakikisha wanamichezo bora wanapata motisha ya kuendelea kufanya vizuri.
The post Waziri Mkuu amkabidhi Alphonce Simbu zawadi ya milioni 20 first appeared on SpotiLEO.