
Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kujenga masoko makubwa mapya matano ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira bora zaidi.
Akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Mwanakwerekwe leo Septemba 29, 2025 katika muendelezo wa kampeni za uchaguzi, Dkt. Mwinyi alisema masoko hayo mapya yatakayojengwa katika maeneo ya Kinyasini, Mwera, Kibandamaiti, Kisauni na Kwahajitumbo yataleta suluhisho la kudumu kwa changamoto za wafanyabiashara.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa masoko hayo kutapunguza msongamano unaotokana na uhaba wa nafasi, pamoja na kupunguza kodi kubwa zinazowakabili wafanyabiashara hivi sasa.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewaomba wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kumchagua tena yeye pamoja na wagombea wa CCM katika ngazi za ubunge, uwakilishi na udiwani, ili kutimiza dhamira ya ujenzi wa masoko hayo chini ya kaulimbiu yake ya “Yajayo ni Neema Zaidi.”
Amesisitiza pia umuhimu wa kudumisha amani ya nchi na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wao.