DAR ES SALAAM:MSANII nyota wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Ali Saleh Kiba maarufu kama King Kiba, amezua gumzo mitandaoni baada ya kumtambulisha rasmi mke wake wa pili kupitia ujumbe maalum wa kumbukizi ya siku ya kuzaliwa.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Alikiba ameandika kwa hisia ujumbe mfupi uliosomeka:
“Happy birthday my wife”,
ambao umeibua hisia mbalimbali kutoka kwa mashabiki na wafuasi wake.
Ujumbe huo umetafsiriwa na wengi kama uthibitisho wa ndoa mpya ya msanii huyo na kuashiria kuwa sasa ameanza ukurasa mpya wa maisha ya ndoa, baada ya kuachana na aliyekuwa mke wake wa kwanza, Amina Khalef kutoka Kenya.
Ali Kiba na Amina walifunga ndoa mwaka 2018 katika hafla iliyohudhuriwa na watu mashuhuri, na walijaliwa watoto wawili. Hata hivyo, ndoa yao ilikumbwa na changamoto na hatimaye kuishia kwa talaka.
Kwa sasa, mke mpya wa Kiba anadaiwa kuwa raia wa Tanzania, ingawa bado taarifa kamili kuhusu jina na maelezo yake binafsi hazijawekwa wazi hadharani.
Katika jamii ya Kiislamu, ambapo Alikiba anatokea, mwanaume anaruhusiwa kuwa na wake hadi wanne endapo ataweza kutenda haki kati yao.
Hivyo, hatua ya Kiba kufunga ndoa ya pili haijawa jambo la kushangaza kwa wengi, bali imechukuliwa kama uamuzi wa kawaida wa maisha kwa mtu mzima.
Mashabiki wake wengi wameendelea kumtakia heri katika hatua hii mpya ya maisha yake ya ndoa.
The post Alikiba amtambulisha mke wa pili rasmi first appeared on SpotiLEO.