Mbeya. Baada ya kufanya kweli katika michezo minne mfululizo ikiwemo mechi za Ligi ya mabingwa Afrika, Yanga imekutana na mlima katika Ligi Kuu Tanzania Bara leo kufuatia suluhu ya bila kufungana dhidi ya Mbeya City.
Hii ni sare ya kwanza kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Roman Falz tangu atambulishwe kikosini msimu huu baada ya kushinda mechi nne ikiwamo ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao, Simba.
Hata hivyo katika hali isiyo ya kawaida baada ya mchezo huo, mashabiki waliripuka kwa shangwe wakiimba maneno ya ‘Hatumtaki, Hatumtaki, hatumtaki, aondoke’ huku uongozi wa Yanga ukijibu kelele hizo.
Timu hizo zilikutana ikiwa zinakumbuka matokeo ya sare ya 3-3 katika mchezo wao wa mwisho uliopigwa Juni 6,2023, ambapo Mbeya City ndio walitangulia mabao matatu na Yanga kusawazisha.
Katika mechi hiyo, mabao ya City yalifungwa na Richardson Ngy’ondya (mawili) na George Sangija huku Bernard Morison (mawili) na Salum Aboubakar wakiisawazishia Yanga.
Msimu huu timu hizo zimeshuka uwanjani ikiwa Yanga ameshinda mmoja dhidi ya Pamba Jiji 3-0 ukiachana na ile ya Ngao ya Jamii walipotakata 1-0 mbele ya watani zao, Simba, huku Mbeya City ikipoteza mmoja mbele ya Azam 0-2 na kushinda bao 0-1 dhidi ya Fountain Gate.
Hata hivyo, Yanga ilikuwa na mwenendo mzuri ikiwa na matokeo ya ushindi wa mechi mbili za ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Willete ya nchini Angola iliyoifunga nyumbani na ugenini kwa jumla ya mabao 5-0 na kuwaondoa kwenye michuano hiyo.
Mechi ilivyokuwa
Dakika tano za kwanza Yanga waliisakama zaidi lango Mbeya City na kuwapa wakati mgumu mabeki na kipa wao Beno Kakolanya.
City waliamka na kuuelewa mchezo na kuamua kufunguka na kufanya mechi kuwa ya kushambuliana, japokuwa Yanga ndio waliingia lango la mpinzani zaidi.
Katika dakika 45 za kwanza Yanga ilipiga kona tatu dhidi ya moja kwa wenyeji, lakini maeneo yote hayakuwa na utulivu katika kutumia nafasi zilizopatikana na kwenda mapumziko bila kufungana.
Mbeya City walipiga mashuti mawili nje ya lango la Yanga na moja ambalo Kipa Djigui Diara aliweza kudaka, huku Kakolanya akiokoa mawili yaliyolenga lango lake na mengine takribani tano yakitoka nje.
Beki wa Mbeya City, Ibrahim Ame alionekana kuwa bora kipindi cha kwanza kutokana na hatari nyingi alizookoa huku Pacome ZouZoua akionekana kuwapa misuko suko City kwa mashambulizi aliyofanya.
Kipindi cha pili Yanga walianza kwa mashambulizi zaidi, ambapo City iliamua kuwapumzisha Willy Mwani aliyeumia na kuingia Peter Mwalyanzi, huku Yanga wakimtoa Doumbia na kuingia Ecua.
Pia Yanga ilifanya mabadiliko, ambapo wachezaji Maxi Nzengeli na Duke Abuya waliwapisha, Kouma na Edmund John katika dakika ya 67 huku Israel Mwenda akimpisha Prince Dube dakika ya 79.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Folz amekubali kukutana na ugumu akieleza kuwa ni sehemu ya matokeo akiahidi kuwa anaenda kusahihisha makosa yaliyojitokeza.
Amesema kwa kuwa ligi inasimama anaenda kuboresha maeneo yote kuhakikisha timu inafanya vizuri haswa mechi za kimataifa zinazoikabili Yanga akiwatuliza mashabiki kuwa wavumilivu.
“Hatukutarajia kupata matokeo haya ila tunakubali yapo makosa ambayo yalionekana upande wa ushambuliaji kushindwa kutumia nafasi tulizopata, tutatumia mapumziko haya kusahihisha,” Amesema Folz.
Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema wamesikia kelele za mashabiki lakini uongozi unaendelea kufanya tathmini na muda ukifika utaamua iwapo utahitajika la kufanya.
Amewaomba mashabiki kuwa watulivu akieleza kuwa timu yao ni bora na Uwanja wa Sokoine umeendelea kuwa mgumu kwao kupata matokeo mazuri.
“Uongozi unaendelea na tathimini kwa hiki kilichosikika kwa mashabiki, tukubali Sokoine kwa historia umeendelea kuwa mgumu kwetu na mambo mengine yatafanyiwa kazi,” Amesema Kamwe.