BRUSSELS: MSHAMBULIAJI Nick Woltemade wa Newcastle United ‘ameoga sifa’ za kocha Eddie Howe, kufuatia mchango wake katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Union Saint-Gilloise kwenye UCL usiku wa Jumatano, siku chache baada ya klabu hiyo kuitwa “wajinga” kwa kumsajili mchezaji huyo kwa dau linachoripotiwa kuwa pauni milioni 65.
Woltemade ndiye aliyefungua karamu ya mabao kwa bao la kwanza kabla Newcastle haijapata ushindi wa nadra ugenini katika michuano ya Ulaya na kujihakikishia pointi zao za kwanza katika msimu huu wa Ligi ya Mabingwa.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 23 alimalizia shuti la Sandro Tonali na kuipatia timu yake bao dakika ya 17, na kuanzia hapo Newcastle walionekana kuwa bora zaidi dhidi ya mabingwa wa Ubelgiji.
“Nadhani amefanya vizuri sana leo kama kawaida yake. Bado naangalia aina yake ya uchezaji kwa sababu tumekuwa na muda mdogo sana wa mazoezi. Lakini unaweza kuona jinsi anavyoshirikiana na wenzake, hilo ni jambo kubwa”.
“Nafikiri uliwaona Anthony wawili (Elanga na Gordon) wakipata mipira mingi kutoka kwake na bila shaka faida hiyo ni kwa timu nzima. Sijui kama atafunga magoli mengi kama hili la leo, kama kweli litahesabiwa kwake, lakini ninafuraha kwa kuwa litamfanya ajisikie amekuwa karibu zaidi na kikosi chetu.” – amesema Howe
Awali, mjumbe wa bodi ya Bayern Munich na mshindi wa Kombe la Dunia, Karl-Heinz Rummenigge, alisema Newcastle ni “wajinga” kwa kukubali dau lililotakiwa na VfB Stuttgart kwa mshambuliaji huyo.
Bayern pia walikuwa na nia ya kumsajili, lakini walijiondoa kutokana na gharama kubwa iliyotajwa na wapinzani wao wa Bundesliga.
Howe aliepuka kujibu moja kwa moja kauli hiyo alipokuwa akizungumza kabla ya mchezo huo Jumanne, akisema: “soko ndilo huamua ada za usajili, na si klabu moja pekee.”
The post Woltemade amkosha kocha Newcastle first appeared on SpotiLEO.