DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Hip Hop nchini, Rosary Robert ‘Rosa Ree’, ameonyesha kutoridhishwa na mwelekeo wa baadhi ya wasanii wenzake, akieleza kusikitishwa na namna wanavyopuuza hali ya kisiasa ilivyo nchini kwa sasa na badala yake kuendelea kutoa nyimbo za mapenzi.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Rosa Ree amesema kuwa huu si wakati wa burudani isiyohusisha uhalisia wa maisha ya Watanzania, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
“Kila nikiingia mtandaoni nikakutana na nyimbo wanazoimba wasanii za mapenzi nashtuka,” ameandika Rosa Ree.
“Kuwapa Watanzania nyimbo za mapenzi wakati kama huu ni kama mtoto akilia ana kiu halafu unamnywesha pombe alewe, alale, ili asikusumbue,” ameongeza kwa hisia.
Msanii huyo ambaye amewahi kujizolea umaarufu kupitia kazi zake zenye ujumbe mzito na mitazamo ya kijamii, amesema kuwa hali hiyo imemfanya mpaka ajutie kuwa msanii ndani ya Tanzania.
Akiendelea kueleza hisia zake, Rosa Ree ameandika:
“Naumia mpaka najishtukia kuitwa msanii wa Tanzania… Ni kwamba hamuelewi? Hamuoni? Mmekua viziwi? Au mmeamua tu kujizima data?”
Amesisitiza kuwa kila kinachoamuliwa katika Taifa kinawahusu Watanzania wote na kama kizazi cha sasa hakitahamasika, basi vizazi vijavyo vitabeba mzigo wa uamuzi wa sasa.
“Ni hivi, kila kinachoamuliwa kwenye Taifa hili, kinatuhusu wote, na msipokionja nyinyi basi watakuja kukionja watoto wenu! Amkeni!” amehitimisha kwa ukali.
The post Rosa Ree alia na nyimbo za mapenzi first appeared on SpotiLEO.