BERLIN: KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani Julian Nagelsmann amesema timu hiyo inalenga kupata ushindi katika mechi zao mbili zijazo za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Luxembourg na Ireland Kaskazini ili kubaki kwenye mbio za kufuzu moja kwa moja kwa Kombe la Dunia la mwakani nchini Canada, Mexico, na Marekani.
Ujerumani wataikaribisha Luxembourg Oktoba 10 kabla ya kusafiri kwenda Belfast siku tatu baadaye kuvaana na Ireland Kaskazini.
Nagelsmann ambaye amemwita mchezaji mpya, beki wa Eintracht Frankfurt Nathaniel Brown, katika kikosi chake cha wachezaji 24, ameshuhudia timu yake ikianza vibaya kampeni zake za Kundi A kwa kupoteza mechi moja na kushinda moja.
Wajerumani hao sasa wako nafasi ya tatu wakiwa na pointi tatu, sawa na Ireland Kaskazini lakini wakibaki nyuma kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Slovakia wanaongoza kundi hilo wakiwa na pointi sita, huku Luxembourg wakiburuza mkia bila pointi.
Timu ya kwanza kutoka kila kundi inafuzu moja kwa moja Kombe la Dunia la 2026 litakaloandaliwa kwa Pamoja na Marekani, Mexico na Canada, huku timu ya pili itacheza playoff.
“Ushindi mara mbili, ndio lengo letu, ili kufuzu moja kwa moja Kombe la Dunia,Hata kama tunawakosa baadhi ya wachezaji, kikosi chetu kina ubora wa kufanya vizuri zaidi kuliko tulivyofanya hivi karibuni.” – alisema Nagelsmann.
Ujerumani walifungwa 2-0 na Slovakia kwenye mechi yao ya kwanza ya Kundi hilo mwezi uliopita, kabla ya kushinda 3-1 nyumbani dhidi ya Ireland Kaskazini.
‘German machines’ Watakosa huduma za beki Antonio Rüdiger na winga Jamal Musiala kutokana na majeraha, lakini Nagelsmann atakuwa na Nico Schlotterbeck kwenye safu ya ulinzi.
Kiungo wa ulinzi wa Bayern Munich, Aleksandar Pavlović, pia amerejeshwa kikosini pamoja na Jonathan Burkardt, huku Nick Woltemade na Maximilian Beier wakijumuishwa miongoni mwa washambuliaji.
The post “Tunataka kushinda mechi zetu” – Nagelsmann first appeared on SpotiLEO.