NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) imeendelea kusalia kuwa asilimia 5.75 katika robo ya nne ya mwaka inayoanza Oktoba hadi Disemba 2025.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema uamuzi huo ulifikiwa na Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) iliyokutana Oktoba 1, 2025, baada ya kubaini kuwa mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 huku uchumi ukiendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha.
“Makadirio ya hivi karibuni kutoka taasisi za kimataifa za Moody’s na Fitch Ratings yameonesha uthabiti wa uchumi wetu. Kwa muktadha huu, Benki Kuu itaendelea kutekeleza sera ya fedha kuhakikisha riba ya mikopo ya siku 7 baina ya mabenki inabaki ndani ya wigo wa asilimia ±2 ya CBR,” amesema Tutuba.
Gavana Tutuba ameeleza kuwa katika robo ya tatu ya mwaka 2025, ukuaji wa uchumi duniani ulipungua kidogo kutokana na migogoro ya kisiasa na changamoto za kibiashara, lakini matarajio yanaonesha kuimarika katika robo ya nne. Bei ya mafuta ghafi ilishuka hadi wastani wa dola 68 kwa pipa, huku dhahabu ikiendelea kuuzwa kwa bei ya juu ya wastani wa dola 3,354 kwa wakia.
Kwa upande wa ndani, amesema mfumuko wa bei Tanzania Bara ulifikia asilimia 3.4 mwezi Agosti 2025, na unatarajiwa kubaki ndani ya lengo la taifa la asilimia 3–5, ukichochewa na utulivu wa thamani ya Shilingi, upatikanaji wa chakula cha kutosha na umeme wa uhakika. Zanzibar nayo ilishuhudia kupungua kwa mfumuko wa bei hadi asilimia 4.0 kutokana na kushuka kwa bei za vyakula.
Aidha amesema kuwa Uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ukilinganishwa na asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2024.
Ukuaji huo ulitokana na sekta za madini, kilimo, huduma za fedha, bima na viwanda. BoT inakadiria uchumi kuendelea kukua kwa zaidi ya asilimia 6 katika robo ya pili na ya tatu ya mwaka huu.
Kwa upande wa Zanzibar, amesema uchumi ulikua kwa asilimia 6.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, huku matarajio ya mwaka mzima yakifikia asilimia 7.3, kutokana na mchango mkubwa wa utalii, kilimo na ujenzi.
Gavana amebainisha kuwa sekta ya kibenki iliendelea kuwa thabiti, yenye mtaji na ukwasi wa kutosha. Mikopo chechefu ilipungua hadi asilimia 3.3 mwezi Agosti 2025, chini ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 5.
“Sekta ya kibenki inazidi kuimarika na kuendelea kutoa mchango chanya katika ukuaji wa uchumi,” amesema.