LONDON: WASHIKA mitutu wa jiji la London Arsenal huenda wakawa wanufaika wakubwa wa mchezo mkubwa wa wikiendi hii kwa kupanda kileleni mwa msimamo wa Premier League Jumamosi, ikiwa Liverpool hawatafanikiwa kuvunja pepo baya la kupoteza michezo mitatu mfululizo dhidi ya Chelsea iliyojaa majeruhi.
Liverpool walipoteza 2-1 dhidi ya Crystal Palace wikiendi iliyopita, kisha wakalazwa 1-0 na Galatasaray kwenye Ligi ya Mabingwa Jumanne, huku pia wakimpoteza kipa wao namba moja, Alisson Becker, kutokana na jeraha. The Reds sasa wanakabiliwa na presha kubwa ya kuzuia msururu wa vichapo kwenye EPL na UCL.
Chelsea, ambao nao wako kwenye hatari ya kupoteza michezo mitatu mfululizo ya ligi, walipata ahueni kwa ushindi mwembamba wa 1-0 nyumbani dhidi ya Benfica kwenye ligi ya mabingwa Jumanne.
Hata hivyo, kikosi cha Enzo Maresca kinaweza kuwakosa hadi wachezaji wanane wa kikosi cha kwanza kwenye mechi hiyo ya Stamford Bridge. Miongoni mwao ni kiungo Cole Palmer anayeuguza jeraha la paja, huku Trevoh Chalobah akisimamishwa baada ya kuoneshwa kadi nyekundu dhidi ya Brighton & Hove Albion.
Kwa upande wa Liverpool, mshambuliaji Mfaransa Hugo Ekitike anaweza kurejea baada ya kuripotiwa kuwa alisumbuliwa na maumivu ya tumbo tu na si jeraha. Aidha, Alexander Isak na Mohamed Salah, waliokaa benchi mwanzoni mwa mchezo wa Istanbul, huenda wakaanza mechi hii.
Arsenal wapo pointi mbili nyuma ya vinara hao na wana idadi nzuri ya mabao. Kikosi cha Mikel Arteta kilishinda 2-1 dhidi ya Newcastle United wikiendi iliopita kupitia bao la kichwa la Gabriel dakika jioni, na kitakuwa nyumbani Jumamosi kumenyana na West Ham United, chini ya kocha mpya Nuno Espirito Santo.
“Ni wazi, Arsenal wako katika kiwango kizuri, Lakini Liverpool wanahitaji kubadili mambo haraka. Ni vigumu kucheza dhidi ya Chelsea, lakini nadhani Reds watashinda 3-1.” – alisema mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Peter Crouch katika podkasti yake.
The post Arsenal yajigeuza ‘Kunguru’ wa Liverpool first appeared on SpotiLEO.