Siku Chache mara baada ya serikali Kuiongeza Kampuni ya Mofat Limited ili kutoa huduma ya usafiri kwenye mradi wa mabasi yaendayo haraka BRT, wananchi wa Jiji la Dar Es salaam wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa hatua za haraka zilizochukuliwa, wakisema kwasasa adha ya usafiri imeisha na hawalazimiki kukaa muda mrefu kwenye Vituo vya daladala pamoja na kupunguza muda wa kukaa Vituoni kwa muda mrefu.
Oktoba 02, 2025 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alitembelea mradi huo wa mabasi yaendayo haraka kwenye Vituo vya Kimara na Kivukoni, akiagiza mabasi 60 yaende kuongeza huduma ya usafiri katika eneo hilo na leo tumefika kwenye baadhi ya Vituo kujionea hali ilivyo baada ya ongezeko la mabasi hayo na kubaini uchache wa abiria kwenye Vituo hivyo tofauti na awali.
Miongoni mwa wananchi hao akiwemo Sikuzani Mohamed Muuzi na Mzee Festo Mbilinyi wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa ongezeko la mabasi hayo, wakisema kwasasa usafiri umekuwa rahisi kwao na hawatumii muda mrefu vituoni kama ilivyokuwa awali, wakilazimika kusubiri basi kwa zaidi ya saa moja.
Wengi wa abiria pia wamesisitiza kuanza kufikiria kuacha magari yao binafsi nyumbani na kuanza kutumia usafiri huo wa umma ambapo katika hatua nyingine abiria wengi pia wameonekana wakipanda mabasi mapya na kuacha yale ya zamani kwa madai tofauti ikiwemo kutaka magari hayo mapya kutokana na kuwa na kiyoyozi, madereva wakionekana kila wakati kuwataka abiria kufunga vioo ili kuruhusu viyoyozi hivyo kufanya kazi vyema.