Msemaji Mkuu wa Serikali, Mhe. Gerson Msigwa, amekanusha taarifa zinazosambaa kuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa umefungwa kwa miezi sita.
“ACHENI KUPOTOSHA.
Hatujatangaza kuufunga Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa miezi 6 kama baadhi ya watu wanavyopotosha.
Tumekaa na TFF na pia timu za Yanga na Simba zilioomba kutumia uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya mechi za ligi na kufanya tathmini ya uharibifu wa sehemu ya kuchezea (pitch) ya uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya mechi mfululizo zilizopita za Kimataifa na za ligi. Tumekubaliana kuwa Yanga na Simba watafute viwanja vingine kwa ajili ya michezo ya ligi na uwanja wa Benjamin Mkapa ubaki kwa ajili ya mechi za Kimataifa, Timu ya Taifa na Dabi mpaka hapo tutakapofanya ukarabati mkubwa wa pitch.
Wale wanaohoji Bilioni 31 zilizotumika kukarabati uwanja, ni hivi ukarabati huo haukuhusisha ukarabati wa pitch. Ulihusisha kuboresha jengo, kuweka mifumo mipya ya umeme na taa, maji, vyoo, njia ya kukimbilia, kuweka viti vyote 62,000, kuweka viyoyozi, mfumo wa sauti, ubao wa matangazo, mabenchi ya ufundi, magoli, kupaka rangi na mfumo wa sauti.
Walioingia Uwanja wa Benjamin Mkapa nambieni kipi hakijafanyika kati ya hivyo?
Pia ni vizuri pia kujua kuwa uwanja mkubwa kama Benjamin Mkapa kila unapotumika ni lazima ufuatiwe na marekebisho kwa sababu hakuna tukio linaloweza kufanya bila kusababisha uharibifu. Na hii sio kwa uwanja huu tu ni viwanja vyote Dunia, na ukarabati wake unahitaji utaalamu na sio kubondabonda.
TAZAMENI PICHA ZA HALI YA UWANJA BAADA YA MECHI 6 MFULULIZO. Na hapo Singida na Azam hawakutumia.
Kumbukeni kulingana na maelekezo ya kitaalamu ya matumizi sahihi ya uwanja wa nyasi halisi (natural grass) uwanja unapaswa kutumika mara mbili au tatu tu kwa wiki. Hope tumeelewana”.Ameandika Msigwa kupitia Instagram yake.