
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mzee Joseph Warioba Butiku amewahimiza Watanzania kuungana na Kauli rasmi iliyotolewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ dhidi ya kulihusisha Jeshi hilo na siasa, akiwaomba kusimama na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya ulinzi na usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mzee Butiku ameyasema hayo Jumapili Oktoba 05, 2025 mbele ya waandishi wa habari Mkoani Mara, akirejea historia ya utumishi wake kwenye siasa, serikalini na Jeshini, akimkana Mwananchi aliyetumia mtandao wa Kijamii kujitambulisha kama Afisa wa Jeshi na kueleza kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania halijawahi kuwa na Afisa asiyekuwa na nidhamu kwa kiwango alichoonesha mtu huyo aliyejiita Kepteni Tesha.
“”Mimi nimepita Jeshini, hatuna uniform ile, kwamba uwe Tanga kwenye joto halafu uvae unifomu mpaka shingoni, kwahiyo yule sio Askari na kama ni askari analo Jeshi lake lingine sio Jeshi la wananchi wa Tanzania na sipendi kuamini wala siamini kwamba ndani ya Jeshi letu tuna watu wa aina hiyo. Jeshi letu ni jeshi la Watanzania, linaongozwa na Rais wetu na Mkuu wa Majeshi na kauli halali zinatoka kule.” Amesema Mzee Butiku.
Katika hatua nyingine Mzee Butiku amewasihi Watanzania kupuuza taarifa zisizotolewa na Viongozi ama mamlaka rasmi hususani wakati huu wa uchaguzi Mkuu, akisisitiza kuwa uchaguzi Mkuu wa Tanzania ni suala la Kikatiba hivyo ni lazima ufanyike kwa kuzingatia sheria na Katiba kama zinavyoeleza.
Katika hatua nyingine Mzee Butiku amewaeleza Watanzania kuwa ni muhimu kukubaliana kwa pamoja na kuyakataa masuala ya kulihusisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ na masuala ya siasa, Kampeni na uchaguzi mkuu, akihimiza kila mmoja kufuata Katiba na sheria vile inavyotaka na kuungana pamoja katika kukemea masuala ya kutaka kuliingiza Jeshi hilo kwenye masuala hayo kwani sio utamaduni wala desturi ya Watanzania.