DAR ES SALAAM:KOCHA mpya wa Simba SC, Dimitar Pantev, amesema kuwa nafasi yake Simba ni changamoto kubwa, lakini anatarajia kuleta mafanikio makubwa msimu huu.
Kocha huyo ambaye ameajiriwa Simba kama Meneja anatokea Gaborone United ya Botswana amekuja kuchukua mikoba ya Fadlu Davids aliyetimkia Morocco.
“Kwanza kabisa ni nafasi na changamoto kubwa kwangu. Simba ni timu kubwa yenye matarajio ya kufanya vizuri kwenye kila michuano. Hakika sio rahisi kuwa hapa, lakini hakuna muda wa kupoteza kwani mchezo ujao wa kimashindano ni siku 10 tu zijazo,” alisema Pantev.
Pantev, mwenye uzoefu mkubwa wa kufundisha klabu mbalimbali barani Afrika, amefundisha timu zaidi ya tano za klabu ikiwa ni pamoja na Gaborone United ya Botswana, ambapo aliongoza msimu wake wa pili kwa mafanikio makubwa.
Kocha huyo aliweka bayana kuwa amechukua nafasi hiyo ili kusaidia Simba kufanya vizuri na ana matumaini kuwa haitachukua muda mrefu kuzoeana na wachezaji na ligi.
“Haikuwa rahisi kuja hapa kwa sababu nilikuwa kwenye mkataba na timu nyingine, na nyaraka zote zilipaswa kuthibitishwa. Matumaini yangu siku zote ni kufanya vizuri,” alisema.
Pantev aliongeza kuwa mipango yake ni kufanya vizuri hatua kwa hatua, kuanzia kuvusha Simba hatua ya makundi kwenye michuano ya kimataifa na kufanya vizuri kwenye ligi ya ndani.
“Najua Simba kwenye misimu miwili mitatu iliyopita hawajawa na misimu mizuri, lakini tunahitaji kufanya makubwa msimu huu na kuwa mabingwa,” alisema.
Kocha huyo pia aliwapa wachezaji na mashabiki wito wa kushirikiana: “Haitakuwa rahisi kwani unakutana na wachezaji ambao hukuwasajili, lakini tupo hapa kufanya kazi. Mashabiki wawe nyuma ya timu yao kwa kujivunia, kwani tupo hapa kuandaa timu vizuri.”
Mwisho
The post Dimitar Pantev: Nimekuja kuisaidia Simba ifanye vizuri first appeared on SpotiLEO.