
Aliyekuwa mmiliki wa Shule ya Sekondari Lilian Kibo High School, marehemu Kibo, aliwahi kutoa wosia wa kipekee kabla ya kifo chake akisema kuwa, “shule hii ni ya Mungu, na endapo nitafariki, ikabidhiwe kwake.”
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Sister Asumpter, ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa shule hiyo, wosia huo ulitekelezwa mara baada ya kifo cha Kibo, na taasisi hiyo ya elimu ilikabidhiwa rasmi kwa Mapadre na Masista kama ishara ya kutimiza matakwa ya marehemu.
Akizungumza na Global TV, Sister Asumpter alielezea historia ya kuvutia kuhusu maisha ya marehemu Kibo na mkewe Lilian, ambao walijitolea kwa moyo mkubwa katika kuanzisha shule hiyo kwa lengo la kutoa elimu bora yenye maadili ya Kikristo.
“Marehemu Kibo na mkewe walikuwa watu wa imani. Walisema wazi kwamba walichojenga hakikuwa chao binafsi, bali ni kazi ya Mungu. Wosia wake ulitekelezwa kwa uaminifu mkubwa,” alisema Sister Asumpter.
Tangu kukabidhiwa kwa Kanisa, shule hiyo imeendelea kuimarika chini ya uongozi wa watawa, ikizingatia maadili, nidhamu na elimu bora kwa wanafunzi wake.