
Jeshi la Polisi nchini limeanza uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa na Augustino Polepole kuhusu madai ya kutekwa kwa ndugu yake, Humphrey Polepole.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi leo Oktoba 7, 2025, jalada la uchunguzi lilifunguliwa mara baada ya taarifa hizo kusambaa jana, Oktoba 6, 2025.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mbali na kukusanya maelezo kutoka kwa watu mbalimbali, Polisi wanaendelea kumtafuta Augustino Polepole ili atoe ushirikiano na maelezo ya kina kuhusu madai hayo, ikiwemo uthibitisho wa madai yake kwamba Afisa wa Polisi alihusika katika tukio hilo.
Aidha, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi pia unalenga kubaini kama kweli Humphrey Polepole alikuwa mkazi au mpangaji wa nyumba ambako inadaiwa tukio hilo lilifanyika.
Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, jijini Dodoma.