
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya Daud Mtuyehabi, aliyewahi kuwa mgombea ubunge kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika Jimbo la Siha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, tukio hilo la kujichukulia sheria mkononi lilitokea usiku wa Oktoba 7, 2025, majira ya saa 1:30 usiku, katika Kijiji cha Kilingi, Kata ya Sanya Juu.
Inadaiwa kuwa, Mtuyehabi alimchoma kisu tumboni Abdul Mohamed, mkazi wa eneo hilo, wakati akiamulia ugomvi uliozuka kati yake na Hamad Mohamed walipokuwa wakinywa pombe, kutokana na kudaiana fedha.
Baada ya tukio hilo, wananchi waliokuwepo eneo hilo waliripotiwa kujichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia Mtuyehabi hadi kusababisha kifo chake.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia watu nane kwa tuhuma za kujihusisha na tukio hilo la mauaji,” imeeleza taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi.
Polisi wamesema uchunguzi wa kina unaendelea, na watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za awali kukamilika.