Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco)Mkoa wa Ruvuma wakipita katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Mbinga kwa ajili ya kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja.
Mkuu wa kitengo uhusiano na huduma kwa wateja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma Allan Njiro kushoto na meneja wa Shirika hilo Wilaya ya Mbinga Mhandisi Edward Kweka kulia,wakimkabidhi jiko mama lishe anayefanya shughuli zake katika maeneo ya Halmashauri ya Mji Mbinga Happy Frank,kama sehemu ya kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ya kupikia na kuacha matumizi ya kuni na mkaa.
………..
Na Mwandishi wetu, Mbinga
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO)Mkoa wa Ruvuma,limeanza kutekeleza kampeni ya kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ya kupikia kwa kugawa majiko ya umeme (Pressuer Cooker)kwa Mama na Baba lishe wanaofanya shughuli zao katika Mji wa Mbinga.
Akizungumza jana Mkuu wa kitengo cha uhusiano na huduma kwa wateja Allan Njiro amesema,Shirika limetoa majiko hayo kama sehemu ya shukurani kwenda kwa jamii iweze kuacha kutumia nishati chafu ya kupikia ya kuni na mkaa.
Aidha alisema, msaada huo wa majiko ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kama nyezo ya kulinda afya za Watanzania,kulinda na kutunza mazingira yetu.
“Katika kutekeleza agizo la Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan,sisi Tanesco tumeona ni vyema kuwawezesha mama lishe ili nao waache kutumia nishati chafu ili kulinda afya zao na kulinda mazingira”alisisitiza Njiro.
Alisema,mpango huo utawawezesha mama lishe kufanya shughuli zao kwa uhakika,ubora,salama na kuhakikisha wanapika chakula cha wateja wao kwa gharama nafuu,usalama na bila kuathiri mazingira.
“Chakula kinachopikwa kwa kutumia majiko haya kinaiva haraka,yanatumia umeme kidogo,salama na yanaokoa sana muda,wakati umefika kwa jamii wakiwemo ndugu zetu mama lishe na jamii kwa ujumla kuachana na matumizi ya kuni na mkaa katika shughuli zao”alisema Njiro.
Kwa mujibu wa Njiro,Tanesco inatambua mchango mkubwa wa mama na baba lishe,hivyo kupitia wiki ya huduma kwa wateja wameamua kurudisha sehemu ya faida wanayopata kuwapa majiko ya umeme baadhi ya mama lishe ili waweze kuboresha shughuli zao.
Njiro alisema,Tanesco itaendelea kutoa majiko katika wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma na mwaka huu wameanza kwa mama lishe na baadhi ya wafanyabiashara wadogo ambao ni watumiaji wa nishati ya umeme katika Wilaya ya Mbinga.
Katika hatua nyingine Njiro alisema,wametoa msaada wa vocha za umeme kwa wamiliki wa Saloon za kiume na kike ikiwa ni kutambua na kuunga mkono kazi wanayofanya kwani umeme ni sehemu ya mtaji katika shughuli zao.
“Tumeamua kuwapa vocha za umeme kulingana na mahitaji yao,Tanesco inatambua hawa ni wadau na watu muhimu kwetu wanaostahili kupata faida katika wiki hii ya huduma kwa wateja”alisema Njiro.
Akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule ya sekondari Mbinga kwa niaba ya Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma Elisius Mhelela, Njiro amewataka wanafunzi na walimu wa shule hiyo kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita kupiga vita matumizi ya nishati ya kuni na mkaa,badala yake wahakikishe wanatumia nishati ya umeme na gesi ili kulinda afya zao na mazingira kwa ujumla.
Njiro, amewaomba kuibeba ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mabalozi wazuri wa nishati safi ya kupikia kwa kutumia majiko ya umeme na gesi.
Mkuu wa Shule Sekondari Mbinga Agapiti Kinunda, ameishukuru Tanesco Mkoa wa Ruvuma kwa kuwajali kwani umeme waliopata kutoka kwa shirika hilo utaongeza hamasa ya wanafunzi has awa kidato cha pili nan ne kusoma kwa bidii wakati huu wakisubiri kufanya mitihani ya Kitaifa.
“Hapa shuleni kuna wanafunzi wanaishi bweni na wale wa kidato cha pili na nne na wale wanaoishi majumbani ambao wanakuja nyakati za usiku kwa ajili ya kujisomea,watapata fursa nzuri na tunatarajia umeme mliotupa utaleta matokeo mazuri kwa vijana wetu”alisema Kinunda.
Naye Mama lishe Happy Frank ameishukuru Tanesco kwa kuwajali na kuongeza kuwa,majiko waliyopewa na Tanesco yatarahisisha kupiga chakula kwa haraka,katika mazingira safi na salama bila kuathiri afya zao na wateja wao.