DAR ES SALAAM:BAADA ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na Rais wa Yanga, Hersi Said kuteuliwa katika kamati tofauti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limewapongeza.
Karia ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Kamati ya FIFA ya Soka la Ufukweni.
Aidha, Hersi ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Klabu za Soka za Wanaume Duniani.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino na kupitishwa na Baraza la Shirikisho hilo jana.
“Hongera Karia na Hersi kwa kuteuliwa na Fifa kwa kipindi cha miaka minne kila mmoja hadi mwaka 2029,”ilisema taarifa hiyo.
Hersi pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA). Katika ukanda wa Afrika Mashariki mwingine aliyeteuliwa ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF), Hussein Mohammed ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Mahusiano ya Kitaasisi wa FIFA.
The post Suala la Karia, Hersi serikali yawapa tano first appeared on SpotiLEO.