Mshambuliaji nyota wa Ureno na klabu ya Al-Nassr, Cristiano Ronaldo
Mshambuliaji nyota wa Ureno na klabu ya Al-Nassr, Cristiano Ronaldo, ametajwa kuwa mchezaji wa kwanza wa soka kufikia hadhi ya bilionea, kwa mujibu wa ripoti mpya ya chombo cha masuala ya fedha, Bloomberg.
Ripoti ya “Bloomberg Billionaires Index”, inayofuatilia watu matajiri zaidi duniani kulingana na thamani yao halisi, imemkadiria Ronaldo kuwa na utajiri unaofikia dola bilioni 1.4 za Marekani (£1.04bn).
Kwa mujibu wa Bloomberg, tathmini hiyo inajumuisha mapato yake ya uwanjani, uwekezaji na mikataba ya matangazo.
Imebainika kuwa Ronaldo alipata zaidi ya dola milioni 550 (£410m) kama mishahara kati ya mwaka 2002 hadi 2023, huku sehemu kubwa ya mapato yake ikitokana na mikataba ya udhamini, ikiwemo ule wa muda mrefu na Nike unaokadiriwa kufikia dola milioni 18 (£13.4m) kwa mwaka.
Ronaldo alipojiunga na Al-Nassr ya Saudi Arabia mwaka 2022, alitajwa kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika historia ya soka, akipokea mshahara wa takriban pauni milioni 177 kwa mwaka.
Mkataba huo, uliotarajiwa kumalizika Juni 2025, umeongezwa kwa miaka miwili zaidi, ukiwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 400 (£298m) — hatua itakayomuweka klabuni hadi atakapotimiza umri wa miaka 42.
Ronaldo, ambaye pia ni mchezaji mwenye wafuasi wengi zaidi duniani kwenye mitandao ya kijamii, anaendelea kuthibitisha kwamba jina lake limekuwa zaidi ya mchezo — ni nembo ya biashara yenye nguvu duniani.