
Johannesburg — Wanaharakati sita wa Afrika Kusini waliokamatwa na Israel walipokuwa wakijaribu kufika Gaza kupitia msafara wa misaada wamesema walitendewa kwa ukatili zaidi kuliko wengine.
Baada ya kurejea nchini, wanaharakati hao walisema walilengwa mara tu maafisa wa Israel walipoona kwamba walitoka Afrika Kusini taifa lililowasilisha kesi ya mauaji ya halaiki dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mwaka 2023.
Mandla Mandela, mjukuu wa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, alisema wanaharakati hao “walitendewa kwa ukatili” kwa sababu serikali yao imechukua msimamo thabiti dhidi ya Israel. “Tulionyeshwa adhabu kwa sababu sisi ni taifa lililothubutu kuipeleka Israel ya ubaguzi wa rangi katika mahakama za kimataifa,” alisema Mandela.
Fatima Hendricks na Zaheera Soomar walisema katika uwanja wa ndege wa OR Tambo kwamba walilazimishwa kuvua hijabu na kuvuliwa nguo mbele ya wanajeshi wa Israel, jambo ambalo halikuwatokea wanawake Waislamu wengine waliokuwa wamekamatwa.
“Vichwa vyetu vilisukumwa ukutani, tukavuliwa nguo kabisa. Ilikuwa ni kwa sababu tulikuwa Waafrika Kusini,” alisema Soomar.
Israel imekanusha madai hayo, ikisema wanaharakati wote walipatiwa fursa ya kuondoka kwa hiari bila kuwekwa kizuizini.
Wanaharakati hao sita walikuwa miongoni mwa watu 450 waliokamatwa wakati jeshi la Israel lilipokamata msafara wa Global Sumud Flotilla — meli 42 zilizokuwa zikijaribu kuvunja ukanda wa baharini wa Israel dhidi ya Gaza na kufikisha misaada ya kibinadamu.
Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV — usisahau ku-like, ku-comment na ku-subscribe ili uendelee kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.