Mfanyakazi wa kitengo cha usafirishaji Tanesco Mkoa wa Ruvuma Mariam Abdul,akimpa Mkuu wa Wilaya ya Songea zawadi ya maua wakati wafanyakazi wa Tanesco walipotembelea Ofisini kwa Mkuu huyo wa Wilaya,kushoto Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Elisius Mhelela.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa)Mhandisi Patrick Kibasa kushoto,akimsikiliza Meneja Uhusiano na huduma kwa wateja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma Allan Njiro, wakati wa ziara ya wafanyakazi wa Tanesco wakiongozwa na Meneja wa Mkoa Mhandisi Elisius Mhelela walipotembelea ofisi za Mamlaka hiyo kwa ajili ya kutoa zawadi na tuzo maalum za kutambua mchango wa Souwasa.
…………..
Na Mwandishi Wetu, Songea
MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile,amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma kutoa huduma bora kwa wananchi,hivyo kuchochea uchumi na kuharakisha maendeleo ya, wilaya, Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Ndile ametoa pongezi hizo jana,wakati akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Shirika hilo wakiongozwa na Meneja wake Mhandisi Elisiu Mhelela waliomtembelea ofisini kwake mjini Songea kwa lengo la kumshukuru kutokana na ofisi yake kuwa na mchango mkubwa kwa Tanesco unaowezesha Shirika hilo kuboresha huduma kwa wateja.
Katika hatua nyingine,Ndile ameitaka Tanesco kufanya uhakiki na kuwafuatilia wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme maeneo ya vijijini na kujiridhisha hasa uhadilifu wa wafanyakazi wao ambao ni kero kubwa kwa kuomba rushwa kwa wananchi wanaohitaji kuunganishiwa umeme.
“Baadhi ya wafanyakazi wa wakandarasi mnaowapa kazi kutekeleza miradi ya umeme vijijini siyo waadilifu,kwani wanaomba rushwa kwa wananchi wanaotaka kuingiziwa umeme kwenye nyumba zao,jambo linalopeleka baadhi ya wananchi kuchelewa kupata umeme”alisema Ndile.
Nayo Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa),imeipongeza Tanesco kuboresha huduma zake ambazo zimewezesha wananchi kupata umeme wa uhakika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Souwasa Mhandisi Patrick Kibasa alisema,Tanesco imekuwa taasisi ya kuigwa inayoshulikia changamoto za wateja wake kwa vitendo.
Alisema,Tanesco imeboresha huduma upatikanaji wa nishati ya umeme katika Mji wa Songea na hali hiyo imetokana na watumishi wa Shirika hilo kufanyakazi kwa kujituma,ushirikiano na weledi mkubwa.
“Tunaona kazi nzuri inayofanywa na wenzetu Tanesco,ni nadra sana katika Mji wetu wa Songea kuona umeme unakatika mara kwa mara,mafaniko haya yanachangiwa sana na uwepo wa watumishi wanaojitambua na wanaofanyakazi kwa kujituma”alisema Kibasa.
Kibasa, amehaidi kuwa Souwasa itaendelea kuwa mteja mzuri kwa kulipa bili za umeme kwa wakati ili kuiwezesha Tanesco kukusanya maduhuli na mapato yatakayosaidia kuongeza na kuboresha huduma zake kwa wateja wake.
Awali Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Elisius Mhelela alisema,Tanesco imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuhakikisha ina boresha huduma kwa wateja hatua ambayo imechangiwa sana uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati.
Mhelela, amewashukuru wadau wote wanaotumia nishati ya umeme katika shughuli mbalimbali, kwani mchango wao umesaidia Shirika hilo kutoa huduma bora kwa Watanzania ambapo lengo la Tanesco ni kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na haraka.
Meneja Uhusiano na huduma kwa wateja Allan Njiro alisema,wataendelea kushirikiana na Souwasa katika kulinda miundombinu na vyanzo vya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji na umeme na kutoa fursa kwao kufanya shughuli za kujiletea maendeleo.
“Vyanzo na miradi ya maji vinahitaji ulinzi mkubwa sana,sisi kama wadau tuna wajibu kuhakikisha tunashirikiana na mamlaka za maji kupeleka nishati ya umeme katika maeneo hayo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi”alisema Njiro.








