Na Mwandishi wetu, Arusha.
Baadhi ya wateja wanaopata huduma mbalimbali ikiwemo za utalii wamejumuika na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika kuhitimisha maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja.
Wakiongozwa na maafisa mbalimbali wa Mamlaka hiyo wadau mbalimbali waliotembelea ofisi za Maelezo (Information Centre) katika Jengo la Ngorongoro Arusha wameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kupokea ushauri kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya utalii na kuufanyia kazi.
Afisa Utalii Mkuu na Masoko wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro bwana Michael Makombe amesema katika kipindi cha siku saba mamlaka imeweza kukutana na wateja na kupokea ushauri kuhusu miundo mbinu,mifumo ya Tehama, Ulinzi na Usalama pamoja na mambo mengine.
Wiki ya huduma kwa wateja huadhimishwa ili kuwaleta pamoja wadau na watoa huduma kwa lengo la kupokea mrejesho wa huduma wanazozitoa ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni Dhamira inayowezekana (Mission Possible)