KAMPENI ya Simba SC ambayo ina lengo la kutokomeza jezi feki inaendelea ambapo Wananchi wamezidi kupewa elimu kuhusu faida za kununua jezi Original.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC ameweka wazi kuwa kununua jezi Original ni jambo ambalo kila Mtanzania anapaswa kujivunia.
Oktoba 9 uongozi wa Simba SC uliweka kambi Mwanza na kutembelea baadhi ya vituo na kuzungumza na Wananchi wa Buhongwa, Nyegezi, Nyamagana, Kisesa na Machinjioni.
Ahmed Ally amesema kuwa kununua jezi feki kunadumaza ustawi wa maendeleo kwa muwekezaji, timu na taifa kiujumla hivyo ni muhimu kununua jezi orijino ambazo zipo kwenye maduka maalumu.
“Hii vita sio nyepesi kila mtu anatafuta njia yake kwenye utafutaji lakini kwa kupitia jezi feki kunaumiza vibaya mno ni hasara kwa muwekezaji, hasara kwa taifa kwa kuwa kuna kodi inakosekana na mapato yanapungua.
“Wanaonunua jezi feki ni wengi lakini pengine inatokea ananunua bila kujua ila kwa sasa ni muhimu kila Mtanzania akafurahia kuvaa kitu orijino hiyo itakuwa ni faida kwake kwa kuwa ameichangia timu yake aipendayo na amechangia kulipa kodi na anachangia maendeleo ya timu.