
Mwanamuziki wa kimataifa wa R&B, Akon, anakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kifamilia na kifedha baada ya mke wake, Tomeka Thiam, kufungua kesi ya talaka kufuatia ndoa yao ya miaka 29.
Kilichowashangaza wengi ni kwamba nyaraka za mahakama zimefichua kuwa Akon ana kiasi cha dola 10,000 (sawa na takribani shilingi milioni 25) pekee katika akaunti yake binafsi.
Vyanzo vya kisheria vimeeleza kuwa Tomeka anadai euro milioni 100 (sawa na shilingi bilioni 245) kama sehemu ya mgawanyo wa mali, akisisitiza kuwa amechangia pakubwa katika kujenga himaya ya kibiashara ya Akon inayohusisha muziki, uwekezaji wa majengo, na mradi wa Akon Lighting Africa.
Hata hivyo, uchunguzi wa mahakama umebaini kuwa mali nyingi hazijasajiliwa kwa jina la Akon bali kwa jina la mama yake, hali ambayo imezua hisia kuwa huenda alihamisha mali hizo ili kujikinga dhidi ya madai ya talaka.
Ufunuo huo umeibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, mashabiki wakijiuliza jinsi msanii maarufu kama Akon anavyoweza kuwa na fedha chache kiasi hicho.
Wengine wanaamini huenda amemchezea mkewe mchezo ili kupunguza kiasi cha mgawanyo wa mali, huku wengine wakiona huenda anakabiliwa na changamoto halisi za kifedha.
Wataalamu wa sheria za ndoa wameonya kuwa kesi hiyo inaweza kuwa ngumu zaidi endapo itathibitishwa kuwa mali nyingi haziko chini ya jina lake kisheria, jambo litakalofanya mgawanyo wa mali kuwa mgumu.
Mpaka sasa, Akon na wawakilishi wake hawajatoa kauli rasmi kuhusu mzozo huo wa kisheria unaoendelea kufuatiliwa kwa karibu na vyombo vya habari.
TAMKO ZITO la JWTZ KUHUSU MAANDAMANO na UCHAGUZI – “WATU WANAOJIITA WANAHARAKATI – WANAPOTOSHA”…