

Jeshi la Polisi Tanzania limetoa kauli kufuatia taarifa zilizotolewa na mwanasiasa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, kupitia mitandao ya kijamii akidai kuwa usalama wake upo hatarini.
Kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa Oktoba 17, 2025, kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dodoma, Msemaji wa Jeshi hilo, DCP David Misime, amesema Polisi wanafuatilia kwa karibu taarifa hizo, huku akimtaka Lema kufika katika kituo cha polisi kilicho karibu naye ili kutoa maelezo rasmi kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
“Tunamsisitiza afike katika Kituo cha Polisi ili awasilishe taarifa yake hiyo rasmi kwa hatua zingine, kwani ndiyo utaratibu wa kisheria,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya Lema kuandika ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram, akiomba ulinzi kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akidai kwamba kuna watu wanaomfuatilia kwa karibu na kuhofia wanaweza kumdhuru.

“Mheshimiwa Rais, maisha yangu yako katika hatari kubwa. Tafadhali, naomba kwa unyenyekevu mkubwa unisikilize. Kwa sasa kuna watu ambao wananifuatilia kwa karibu sana. Hata jioni ya leo wameonekana maeneo ya nyumbani kwangu, na nina hofu kwamba wangeweza hata kumdhuru mtu yeyote ambaye si mimi,” aliandika Lema.
Katika ujumbe huo, Lema aliongeza kuwa kutokana na hofu hiyo, anaona ni bora awekwe mahabusu kwa hiari hadi kipindi cha uchaguzi kipite, ili kulinda usalama wake pamoja na familia yake.
Jeshi la Polisi, kupitia taarifa hiyo, limewataka viongozi wa kisiasa na wananchi kwa ujumla kuzingatia utaratibu wa kisheria katika utoaji wa taarifa zinazohusu usalama au matishio, ili kuepusha taharahuki na upotoshaji usio wa lazima katika jamii.
“Tunasisitiza kila mwananchi kufuata utaratibu wa kisheria katika kutoa taarifa sahihi kwa mamlaka husika za haki jinai,” limeeleza Jeshi hilo.
Kwa mujibu wa Polisi, uchunguzi unaendelea kubaini ukweli wa madai hayo, huku likisisitiza kwamba usalama wa raia wote nchini uko chini ya ulinzi wa vyombo vya dola na hakuna raia anayeachwa bila ulinzi kwa misingi ya itikadi au nafasi yake ya kisiasa.