UONGOZI wa Yanga umeanza upya mchakato wa kutafuta kocha wa timu hiyo baada ya kufunga uwezekano wa kumchukua kocha Romuald Rakotondrabe ‘Roro’ aliyekuwa anakaribia kutua katika timu hiyo, huku Nasreddine Nabi akitia mkono.
Uamuzi huo unakuja baada ya Yanga kuachana na aliyekuwa kocha wao Romain Folz, baada ya timu hiyo kupoteza mechi ya kwanza msimu huu ikifungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Silver Strikers ya Malawi.
Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imeiweka Yanga kwenye nafasi ya kutakiwa lazima ishinde angalau kwa tofauti ya mabao 2-0 katika mechi ya marudiano itakayopigwa Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Folz ambaye ameiongoza Yanga kwenye mechi sita za mashindano, ameshinda nne na sare moja, timu yake ikifunga mabao tisa huku bao pekee ililoruhusu Malawi ndio lililohitimisha maisha yake ndani ya klabu hiyo, akichukua taji moja la Ngao ya Jamii.
Timu hiyo sasa itakuwa chini ya kocha Patrick Mabedi aliyekuwa msaidizi wa Folz wakati Yanga ikitafuta kocha mpya wa kuendelea na majukumu ya kukinoa kikosi hicho.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa juu wa Yanga ni kwamba, klabu hiyo haitaendelea na hesabu za kumchukua Roro ambapo mchakato huo umegeuziwa kwa kocha mpya mwingine.
Bosi mmoja wa juu amesema kuwa mchakato wa Roro hautaendelea kufuatia uongozi wao kuachana naye kwa sababu ambazo hata hivyo hawakutaka kuziweka wazi.
“Ni kweli tulikuwa na hesabu za kumchukua kocha Rakotondrabe (Roro) lakini kuna mambo yametupa wasiwasi, hatutaweza kuendelea na huo mpango tena,” amesema bosi huyo.
“Tutarudi kuanza mchakato upya kabisa, tunataka kufanya mambo kwa umakini zaidi, tupate kocha ambaye atatupa kile ambacho tunakitarajia kama klabu.”
Kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi akizungumzia hilo, ameitaja Yanga kuwa makini kwenye mchakato wa kupata kocha mpya akisema wanahitaji kocha mwenye ufundi wa kisasa utakaoiruhusu timu kujenga mashambulizi.
Nabi aliyeifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023, amesema hana shida na ubora wa wachezaji wa kikosi hicho, lakini akasema inahitajika kocha ambaye ataweza kuwalazimisha wachezaji kujituma na kutekeleza ipasavyo yale ambayo yanatakiwa.
“Sio taarifa nzuri kwa Yanga kupoteza kocha wakati huu, kuna presha inaongezeka kwa uongozi na hata timu, lakini naamini wanaweza kurudi kwenye utulivu. Siku zote naamini katika hatua zao,” amesema Nabi, ambaye hivi karibuni ameachana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
“Nilikuwa hapo Tanzania, niliwaona (Yanga) sina tatizo na ubora wa wachezaji wao hata kocha, lakini nadhani wanahitaji kocha mwenye uzoefu mkubwa anayeweza kuisimamia klabu yenye presha ya matokeo kama Yanga.
“Nilivyowaona ni kama wachezaji walikuwa hawaogopi kucheza nje ya maelekezo, wanahitaji kocha ambaye akiwa nje amesimama wachezaji wake watakuwa wanakumbuka kile wanachotakiwa kufanya.”
The post KUHUSU KOCHA MPYA YANGA….NABI ATIA NENO…ATOA TAHADHARI MAPEMAAA….. appeared first on Soka La Bongo.