Na Silivia Amandius
Bukoba.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kagera imewapatia semina ya elimu kuhusu masuala ya kodi na dawati maalumu la uwezeshaji biashara, Maafisa Watendaji wa kata zote 14, mitaa 66 pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii 16 wa Manispaa ya Bukoba.
Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Stella Hotel mjini Bukoba, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, ambaye amepiga marufuku watumishi wa umma kuwakingia kifua wafanyabiashara wanaokwepa kodi.
Sima amesema ni muhimu watendaji kushirikiana na TRA ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake bila vikwazo, na ameonya kuwa mtumishi yeyote atakayebainika kumkingia kifua mfanyabiashara anayekwepa kodi atachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Huduma kwa Mlipa Kodi wa TRA Mkoa wa Kagera amesema kuwa zaidi ya asilimia 30 ya uchumi wa taifa unaendeshwa na sekta isiyo rasmi, hali ambayo inachangia kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji kodi katika eneo hilo.
Aidha, serikali kupitia mwaka wa fedha 2025/2026 imeipa TRA lengo la kusajiri namba mpya za utambulisho wa mlipakodi (TIN) zipatazo milioni moja nchini. Mkoa wa Kagera umepewa lengo la kupata walipa kodi 20,000, ambapo hadi sasa ni walipa kodi 6,641 pekee wenye TIN za biashara na zisizo za biashara. Serikali imepanga kuongeza usajiri wa TIN zipatazo 14,328 katika mkoa huo.
Amesema lengo kuu ni kuendelea kushirikiana na watendaji wa kata na mitaa kuhakikisha biashara zote zinasajiliwa, zinatambulika, na wamiliki wake wanalipa kodi kwa wakati ili kuchochea maendeleo ya taifa.
Nao baadhi ya washiriki wa semina hiyo akiwemo Godi Michael Wambuga na Esther Christopher Mbatila, wamesema wamepata uelewa mkubwa kuhusu wajibu wao katika kushirikiana na TRA kuhakikisha wafanyabiashara wanalipa kodi kwa wakati kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.