Na: Dkt. Reubeni Lumbagala
Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni moja ya Jumuiya muhimu kwa uhai na maendeleo ya CCM. Misingi mikuu ya Jumuiya hii kutoa elimu na malezi kwa jamii.
Elimu ni nyenzo muhimu katika kujenga ustawi na maendeleo ya jamii. Ili jamii ipige hatua za kimaendeleo suala la elimu haliepukiki. Jumuiya ya Wazazi licha ya kuwa ni Jumuiya ya kisiasa lakini inatoa elimu ya masuala mbalimbali katika jamii. Kwa kutambua umuhimu wa elimu katika jamii, Jumuiya hii ina miliki shule zake ili kuchagiza vizuri msingi wake wa kutoa elimu kwa jamii.
Sambamba na hilo, Jumuiya hii pia imejengwa katika msingi wa kutoa malezi kwa jamii juu ya masuala mbalimbali muhimu katika jamii. Malezi bora katika jamii yanasaidia kujenga jamii yenye raia wenye maadili mazuri na wanaowajibika, hivyo kusaidia katika kufanikisha maendeleo.
Jumatano ya Oktoba 29, 2025, ni siku muhimu kwa nchi yetu ya Tanzania. Ni siku ya Uchaguzi Mkuu. Wananchi wanapata fursa ya kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa. Wananchi watapiga kura kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
Kutokana na umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi huu, Jumuiya ya Wazazi ya CCM imekuja na kampeni yake ya kuhamaisha wananchi kujitokeza kupiga kura siku ya Oktoba 29. Kampeni hii imepewa jina la “Nipitie Tukatiki.” Kampeni hii inatoa rai kwa mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura aliyejiandikisha kupiga kura kumpitia ndugu, jamaa au rafiki yake ili waongozane kwa pamoja kwenda kupiga kura.
Nipitie Tukatiki inatukumbusha umuhimu wa wananchi kuungana kwa pamoja kwenda kutimiza haki ya kikatiba ya kuchagua viongozi watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo yaani 2025-2030. Hivyo basi, ni vyema siku ya Oktoba 29, kumpitia ndugu, jamaa na rafiki yako ili kuambatana kwa pamoja kwenda kupiga kura.
Kwa familia na wanandugu wanaoishi nyumba moja ni vyema kutoka kwa pamoja kwenda kupiga kura. Kampeni hii ya Nipitie Tukatiki imekuja wakati sahihi hasa kuelekea Oktoba 29, ambayo ni siku muhimu ya kufanya maamuzi sahihi kwa maendeleo ya nchi yetu. Kwa mustakabali mwema wa maendeleo, usiende mwenyewe kupiga kura, mpitie mwenzio, mkapige kura Oktoba 29.
Dkt. Reubeni Lumbagala ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800462