DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga imetangaza kuwa, mechi zake za nyumbani katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu itatumia Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar.
Ni wazi sasa Yanga itaungana na wanalambalamba wa Chamazi Azam FC na Singida Black Stars Kwenda Zanzibar ambao pia, walitangaza kutumia Uwanja huo kwa mechi zao za Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na waandishi wa Habari Dar es Salaam leo Ofisa Habari wa Yanga Ally Kamwe alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kuzingatia maslahi mapana ya timu, mashabiki na mazingira bora ya kiuchezaji.
“Baada ya uongozi kufanya tathmini na kuangalia maslahi mapana ya klabu yetu, napenda kuwatangazia kuwa mechi zetu zote tatu za nyumbani kwenye hatua ya makundi tutatumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar,” alisema Kamwe.
Aliongeza kuwa maandalizi makubwa yanaendelea kuelekea mchezo wa kwanza wa nyumbani dhidi ya FAR Rabat ya Morocco, na akawataka mashabiki wa visiwani kujiandaa kuipokea timu kwa nguvu kubwa.
“Niwaombe sana mashabiki na wanachama wetu kutoka visiwa vya Pemba na Unguja kujiandaa kuipokea timu. Pia, wanachama wetu wa Tanzania Bara wajipange kuisapoti timu, maana tupo kwenye kundi gumu, lakini tukiwa wamoja tutafanikiwa,” alisisitiza Kamwe.
Katika hatua nyingine, kikosi cha timu hiyo kimerudi kambini jana na kimeanza maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC FC, utakaopigwa Novemba 9 katika Uwanja wa KMC.
Aidha, mchezo dhidi ya Prisons SC uliokuwa umepangwa kufanyika jijini Dodoma umeahirishwa, na klabu hiyo inasubiri tarehe mpya kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB).
Mwisho
The post Yanga yazifuata Azam, Singida New Amaan first appeared on SpotiLEO.



