Mshambuliaji wa Yanga SC, Clement Mzize, ataukosa mchezo ujao wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC FC utakaopigwa Novemba 9, 2025 saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, kutokana na majeraha ya goti.
Mzize, ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu, anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki nane hadi kumi, hali inayomfanya kukosa michezo kadhaa muhimu ya ligi.
Nyota huyo pia alikosekana katika mchezo uliopita ambapo Yanga SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Oktoba 28, 2025 kwenye uwanja huohuo, mabao yakifungwa na Zimbwe Jr pamoja na Ecua.
Kutokana na kukosekana kwake, mabingwa hao watetezi wameendelea kumtegemea mshambuliaji Prince Dube, ambaye bado hajaonyesha kiwango chake cha kilele tangu kurejea uwanjani. Dube alianza katika kikosi cha kwanza mchezo uliopita lakini alishindwa kukamilisha dakika 90.
Yanga SC inaingia katika mchezo ujao dhidi ya KMC ikitafuta kuendeleza rekodi yake nzuri ya matokeo, huku benchi la ufundi likikabiliwa na jukumu la kuhakikisha pengo la Mzize halitahiri mwendelezo wa ushindi.



