NAIROBI: MSANII na mjasiriamali wa muziki nchini Kenya Sironka Lioness amezindua rasmi, kituo kipya cha ubunifu chenye lengo la kukuza na kuwawezesha vijana wenye vipaji katika tasnia ya burudani nchini.
Sironka alisema mradi huo wa Studio ya Lioness Empire ni matokeo ya miaka ya kujituma, kujinyima, na kuamini katika ndoto zake.
“Nimewekeza katika mradi huu baada ya ziara yangu ya muziki barani Ulaya. Shauku yangu ni kuona vijana chipukizi wakifikia ndoto zao na kupata tumaini,” alisema.
Studio hizo, zilizojengwa kwenye eneo lake binafsi kando ya barabara ya Kangundo, Embakasi East, zimejengwa kwa viwango vya kimataifa, zikiwa na vifaa vya kisasa vya kurekodi sauti, vyumba vyenye ubora wa juu wa sauti (acoustic rooms) na sehemu kamili za uzalishaji muziki.
Ingawa hakutaka kufichua gharama kamili ya mradi huo, Sironka alidokeza kuwa amewekeza kiasi kikubwa caha fedha katrika maradi huo.
Kutoka kwenye booth za kurekodi zenye muundo wa kisasa hadi maeneo ya kuhariri na maonesho ya moja kwa moja, Lioness Empire Studios inatoa mazingira bora na ya kuvutia kwa wasanii, watayarishaji na wabunifu kufanya kazi kwa ushirikiano na ubunifu.
Kabla ya kurejea kikamilifu kwenye muziki, Sironka aliwahi kufanya kazi katika sekta ya elimu, lakini mwaka 2018 alifanya uamuzi wa kuacha kazi na kujikita kwenye sanaa.
Mbali na studio, Sironka pia anaendesha kipindi chake cha mahojiano kiitwacho Lioness Sayso Talk Show, ambacho huwapa vijana wabunifu na wavumbuzi nafasi ya kujitangaza bila malipo.
“Mahojiano haya hayana gharama. Ninapenda kuona vijana waking’aa. Mimi ni mtumishi tu niliyeitwa kwa kusudi,” aliongeza.
Kipindi hicho, ambacho huandaa hadi mahojiano 60 kila wikendi, kimekuwa jukwaa muhimu la kusimulia hadithi za kweli na kuhamasisha jamii, likiongeza zaidi ushawishi wake katika ulimwengu wa ubunifu.
Kuhusu muziki wake, Sironka alisisitiza kwamba hajauacha muziki, bali amepumzika kwa muda ili kuimarisha chapa ya kipindi chake cha mahojiano.
“Muziki bado upo. Kuandaa vipindi ni wito wangu pia,” alisema.
The post Sironka azindua studio ya kisasa kusaidia vijana first appeared on SpotiLEO.






