DAR ES SALAAM: WEKUNDU wa Msimbazi Simba na watani zao Yanga wanarudi Uwanjani Jumamosi na Jumapili katika michezo ya Ligi Kuu baada ya mara ya mwisho kutoka katika michezo ya kimataifa.
Timu zote mbili zimetoka kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa zinaelekeza nguvu michezo ijayo ya ligi kabla ya kuanza tena kampeni za makundi.
Simba itakuwa ugenini Jumamosi dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Dar es Salaam. Simba ilicheza michezo miwili ya ligi dhidi ya Fountain Gate na Namungo na kushinda mabao 3-0 kwa kila mchezo.
Wanashika nafasi ya saba kwa pointi sita, watahitaji ushindi kupanda nafasi za juu. Wapinzani wao JKT Tanzania katika michezo mitano, imeshinda mmoja na sare nne ikishika nafasi ya tano. Nao pia, wanahitaji ushindi kuwa katika mazingira mazuri.
Yanga itacheza Jumapili dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam. Mpaka sasa wamecheza michezo mitatu na kati ya hiyo, wameshinda miwili na sare moja.
KMC wanashika mkia ambapo wamecheza michezo mitano na kati ya hiyo, wameshinda mmoja na kupoteza minne hivyo, bado wanapambana kutafuta matokeo mazuri kujiondoa walipo wakati wenzao wanataka kuwa katika nafasi za juu.
Vigogo wengine watakaokuwa Uwanjani Jumamosi ni Singida Black Stars dhidi ya Pamba huku Azam FC ikitarajiwa kucheza Jumapili dhidi ya Namungo.
The post Simba, Yanga kurudi Uwanjani wikiendi hii first appeared on SpotiLEO.





