Msimu wa 2025/26 umeendelea kuwa mgumu kwa mshambuliaji wa Simba SC, Steven Mukwala, ambaye bado hajafanikiwa kufungua akaunti ya mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mukwala hajaonyesha ubora unaotarajiwa kutoka kwake, licha ya kupata nafasi kadhaa za kufunga katika mechi za ushindani. Kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Novemba 8, 2025, straika huyo alikosa nafasi tatu za wazi, moja kati ya hizo ikiwa ni clear chance ambayo alishindwa kutumia vyema na badala yake kumpasia mlinda mlango wa JKT Tanzania aliyeokoa hatari hiyo.
Mchezaji huyo alitumia dakika 60 uwanjani kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Jonathan Sowah, ambaye alifunga bao la ushindi kwa kutumia pasi safi kutoka kwa kiungo mshambuliaji Morice Abraham.
Kwa sasa, Simba SC ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi baada ya michezo mitatu, ikiwa imefunga jumla ya mabao nane na kukusanya pointi tisa. Mukwala amecheza mechi mbili kati ya tatu za msimu huu, huku akikosekana katika mchezo mmoja.




