AHMED Ally, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba SC, ameweka wazi kuwa tofauti ya pointi kwenye msimamo wa ligi inasababishwa na idadi ya mechi ambazo timu zimecheza.
Kwa mujibu wa mwenendo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2025/26, vinara kwa sasa ni Yanga SC inayoongozwa na Kocha Pedro Gonçalves, ikiwa imecheza michezo minne na kujikusanyia pointi 10.
Simba SC inashika nafasi ya pili, ikiwa imeshuka dimbani mara tatu pekee sawa na dakika 270, na imekusanya jumla ya pointi 9.
Mchezo wao wa mwisho kabla ya ligi kusimama ulikuwa dhidi ya JKT Tanzania ugenini, ambapo Simba ilipata ushindi wa 2-1. Katika mchezo huo, bao la JKT lilifungwa na Edward Songo, huku mabao ya Simba yakifumwa kimiani na Wilson Nangu pamoja na Jonathan Sowah.
Akizungumzia hali ilivyo kwenye msimamo, Ahmed Ally alisema:
“Msimu huu tumejitahidi sana kutafuta matokeo kwenye kila mchezo. Ikiwa unaona timu fulani inaongoza kwa sasa, ni kwa sababu imetushinda kwenye idadi ya mechi ilizocheza. Lakini upande wa matokeo tumeonyesha uimara mkubwa.”



