Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe akizungumza wakati akishiriki uzinduzi wa mpango wa nishati safi ya kupikia shuleni ambao unalenga kuziwezesha taasisi hizo za elimu kutumia nishati safi ya kupikia, uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil.
NAIBU Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe amewaomba wadau wa maendeleo kuendelea kuchangia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini Tanzania ili kuwawezesha wananchi kuacha kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa hivyo kulinda afya na mazingira.
Ametoa wito huo wakati akishiriki uzinduzi wa mpango wa nishati safi ya kupikia shuleni ambao unalenga kuziwezesha taasisi hizo za elimu kutumia nishati safi ya kupikia, uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi ya kupikia ameonesha dhamira ya dhati ya kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo.
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia amekuwa akichagiza ‘Agenda 300’ ambayo inalenga kupeleka umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030 hivyo itasaidia wananchi kutumia umeme wa gharama nafuu na kuacha kutumia nishati isiyo rafiki kwa mazingira.
Prof. Msoffe amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili kumuwezesha kila Mtanzania kumudu.
Amesema kuwa pamoja na Serikali kutoa maelekezo kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuachana na kuni na mkaa, inaendelea kuchagiza elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia.
Pia, ameeleza kuwa bado wananchi wanahitaji kupata nishati safi ya kupikia ambapo inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi na kuachana na kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.
Aidha, Prof. Msoffe amewashukuru wadau wa maendeleo wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) kwa kuanzisha program hii kwenye shule na kuwahakikishia Tanzania itaendelea kuwapa ushirikiano ili kuleta maendeleo endelevu.
Amesema mpango huo si tu unaziwezesha shule kupata nishati safi ya kupikia bali pia unawajenga wanafunzi kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa jamii inayowazunguka.
Kwa upande wake Mshauri wa Masuala ya Nishati kutoka WFP Tanzania Bw. Geofrey Ndegwa WFP amesema shule ni sehemu muhimu ya kuwekeza agenda ya nishati safi ya kupikia kwani wanafunzi wanapata ufahamu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo.
Amepongeza juhudi za Serikali za kuhakikisha taasisi zote za elimu zinaanza kutumia nishati safi ya kupikia kwakuwa zinahudumia idadi kubwa ya watu (Zaidi ya 100) hivyo kutumia kuni na mkaa kwa wingi na kusababisha miti kukatwa kwa wingi.
Bw. Ndegwa ametoa wito kwa Serikali kushirikiana na wadau wakiwemo Shirika la WFP katika kuchagiza agenda ya nishati safi ya kupikia katika shule zote hatua itakayosaida kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na ukataji wa miti.
Nae Profesa Ed Brown kutoka Program ya Moden Energy Cooking Service amesema kuna fursa kubwa katika kuziwezesha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kupata nishati safi ya kupikia.
Amesema ni wakati sasa sekta binafsi zikashirikiana na Serikali katika kuhakikisha agenda ya nishati safi ya kupikia inakua na kusambaa kwa jamii.


.jpg)


.jpg)
.jpg)



