Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Kyela Bi. Victoria Swebe, mkazi wa Lubele na wenzake watatu ambao ni Bryson Kamembe, Asajile Mwasalemba na Elia Mwalumbu wote wakazi wa Wilayani Kyela Mkoani Mbeya.
Watuhumiwa kwa pamoja wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za uchochezi.
Upelelezi unakamilishwa ili hatua nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao na wanaoshirikiana nao.
AMUUA MTOTO WAKE KISHA NA YEYE KUJINYONGA KWA KAMBA.
Mnamo Novemba 18, 2025 saa 3:00 asubuhi huko Kitongoji na Kijiji cha Isaka, Kata ya Nkunga, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya. Mtoto mwenye umri wa miaka 02 aitwaye Devina Derick Iman aliyekuwa mkazi wa Kitongoji cha Ipoma alinyongwa hadi kufa kwa kutumia Kamba ya Manila na Baba yake mzazi aitwaye Derick Iman Mwangama [23] mkazi wa Kijiji cha Mpandapanda Wilayani Rungwe.
Awali kabla ya tukio, Baba mzazi wa mtoto huyo alikwenda nyumbani kwa mama mzazi wa mtoto aitwaye Violeth Edward [19] Mkazi wa Isaka na kumchukua mtoto huyo kwa nguvu na kisha kutokomea kusikojulikana hadi alipokutwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa kando ya Mto Kiwira.
Aidha, baada ya tukio hilo Derick Iman Mwangama naye alijinyonga hadi kufa kwa kutumia Kamba ya Manila kwenye mti wa mparachichi kando kando ya mwili wa mtoto wake.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia baina ya wazazi wa mtoto huyo ambao wametengana.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wazazi kutatua migogoro yao ya kifamilia kwa njia sahihi kwa kushirikisha watu wa karibu na kukaa meza ya mazungumzo ili kupata suluhisho kwa njia ya Amani na kuepusha madhara makubwa kama haya yaliyotokea.
Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.




