MANCHESTER: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, amesisitiza Ijumaa hii kwamba msimu halisi ndo unaanza sasa huku timu yake sasa ikipambanai kupunguza gepu na kuwapita Arsenal kileleni mwa Ligi Kuu ya England (Premier League).
City walifanikiwa kupunguza pengo la pointi na vinara Arsenal hadi kufikia nne kabla ya mapumziko ya kimataifa yaliyomalizika. Hii ilitokana na ushindi wao wa 3-0 dhidi ya Liverpool, baada ya Arsenal kudondosha pointi katika sare ya 2-2 dhidi ya Sunderland.
Akiongea kabla ya mechi ya timu yake dhidi ya Newcastle kesho Jumamosi, Guardiola aliulizwa kuhusu umuhimu wa mabadiliko ya kasi yanayoweza kutokana na matokeo hayo. Kocha huyo alikiri kuwa ni muhimu kutowaruhusu Arsenal, kujenga pengo kubwa zaidi. Hata hivyo, alisisitiza kuwa msimu bado ni mchanga.

“Hisia niliyokuwa nayo huko nyuma tulipopambana sana dhidi ya Liverpool, nilihisi kwamba hatutaacha pointi nyingi na wakichukua umbali mkubwa, itakuwa ngumu kuwafikiaIlikuwa sawa na Liverpool msimu uliopita, ambapo walikuwa mabingwa ligi zikiwa zimesalia mechi nne.” – amesema.
Guardiola, ambaye ameshinda taji la Premier League mara sita akiwa na Manchester City, alisema kuwa hakuna kitu kitakachoamuliwa mwezi Novemba. Akieleza msimu wa soka una sehemu mbili muhimu, baada ya dirisha la usajili na baada ya mapumziko ya kimataifa.
“Sasa mapumziko ya kimataifa yamekwisha, kwa hivyo tutakuwa pamoja hadi Machi, tukionana kila baada ya siku tatu, nne. Sasa ndio msimu unaanza. Na jambo muhimu ni kuwepo huko, kuwa karibu huko na baada ya hapo kufika mwishoni mwa msimu tukiwa na nafasi ya kuweza kulipigania taji. Hilo ndilo lengo na bila shaka kushinda kesho itakuwa hatua muhimu kwetu.” aliongeza

Ikiwa City wataifunga Newcastle ya Eddie Howe, ambayo inajipapatua, watapunguza pengo na kubaki pointi moja tu nyuma ya Arsenal. Arsenal watacheza nyumbani dhidi ya mahasimu wao wa London, Tottenham, Jumapili.
Guardiola alithibitisha kwamba City watawakosa wachezaji wao wawili muhimu, Mateo Kovacic na Rodri, katika safari yao ya St James’ Park.
“Kila mtu yuko sawa isipokuwa Kova na Rodri. Rodri anapiga hatua nzuri ni karibu wiki tatu tangu apate tena matatizo. Anajua anapaswa kuchukua muda kupona vizuri kiakili na kimwili na kuwa thabiti kuanzia sasa hadi mwisho.” – alisema.
The post “Tunaanza msimu sasa” – Guardiola first appeared on SpotiLEO.





