MUMBAI: GWIJI wa filamu za Bollywood, KewalKrishan Deol amefariki dunia asubuhi ya leo Jumatatu, Novemba 24 akiwa na umri wa miaka 89.
Habari za kifo chake zimelitikisa jiji la Mumbai na ulimwengu mzima wa filamu, hasa ikizingatiwa kuwa wiki moja tu iliyopita alikuwa ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Breach Candy baada ya kutibiwa kwa zaidi ya wiki mbili.
Alfajiri ya Jumatatu, jamaa na marafiki wa karibu waliwasili katika viwanja vya krematorium ya Pawan Hans, ambako mwili wa nyota huyo ulipelekwa kwa ajili ya taratibu za mwisho.
Hali ya gwiji huyo ilizidi kuwa mbaya mwishoni mwa wiki, na Jumatatu alfajiri alipumua pumzi yake ya mwisho akiwa nyumbani, akiwa amezungukwa na familia yake.
Hema Malini mke wa Dharmendra ameumizwa zaidia kwani yeye ndiye aliyeongozana na mumewe kumrudisha nyumbani baada ya kuwa katika hali ya kuridhisha wiki mbili zilizopita.
Katika siku za mwisho za uhai wake, Dharmendra alitembelewa na nyota kadhaa wa filamu, akiwemo Shah Rukh Khan, Salman Khan na Aamir Khan, waliokwenda kumuona waliposikia kuhusu hali yake.
Kwa zaidi ya miaka 60 katika taaluma ya uigizaji, Dharmendra alitoa mchango mkubwa katika filamu kama ‘Ayee Milan Ki Bela’, ‘Phool Aur Patthar’, ‘Seeta Aur Geeta’, ‘Jugnu’, ‘Yaadon Ki Baaraat’, ‘Dost’, ‘Sholay’, na nyingine nyingi zilizompa heshima kubwa katika tasnia ya filamu za Kihindi. Ingawa alijaliwa mafanikio makubwa, mara nyingi alionekana kama shujaa wa watu wa kawaida na hilo ndilo lililomfanya kuwa kipenzi cha wengi.
Tasnia ya filamu na Bollywood kwa ujumla imempoteza mwamba, msanii mwenye moyo, na mhimili wa vizazi vingi katika sanaa ya filamu za Kihindi.
The post Gwiji la filamu za India Dharmendra amefariki dunia first appeared on SpotiLEO.



