DAR ES SALAAM: MSEMAJI wa Azam FC, Hasheem Ibwe, amesema kikosi chao kimejipanga kikamilifu visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mchezo muhimu wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Wydad Athletic Club ya Morocco.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Ijumaa, Novemba 28, Ibwe amesema Wydad ni moja ya timu ngumu barani Afrika na si rahisi kukabiliana nayo, hasa ikizingatiwa wametoka kushinda mchezo wao wa kwanza dhidi ya Nairobi United.
“Wydad sio timu nyepesi kukabiliana nayo. Tunajua ukubwa wao na uzoefu walionao. Lakini sisi tuko tayari. Hatuendi kucheza kwa mzaha, haya ni mashindano magumu,” amesema Ibwe.
Amesema licha ya Azam FC kupoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Maniema Union ya DR Congo, morali ya wachezaji imeendelea kuwa juu na kikosi kimejifunza kutokana na makosa yaliyofanywa.
“Tumetoka kupoteza dhidi ya Maniema lakini hatujakata tamaa. Tunarudisha nguvu, tumefanya marekebisho na tunaingia kwenye mchezo wa pili tukiwa na imani kubwa kwamba tutafanya vizuri mbele ya mashabiki wetu,” amesema.
Ibwe ameongeza kuwa mchezo wa nyumbani unaweza kuleta mabadiliko makubwa, akisisitiza kuwa Azam FC imejiandaa kupambana na inaweza kuishangaza Wydad licha ya wengi kuipa nafasi timu hiyo ya Morocco.
“Tunajua Wydad ni kigogo, wengi wanaipa nafasi. Lakini bado chochote kinaweza kutokea. Tunaweza kuwashangaza kwenye uwanja wa nyumbani,” amesema msemaji huyo.
Azam FC inahitaji ushindi ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, ambapo mashabiki wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu yao.
The post Azam FC yaapa kuwashangaza Wydad first appeared on SpotiLEO.


