DAR ES SALAAM: SIMBA SC imeweka pembeni machungu ya kupoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico, baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0, na sasa macho yote yameelekezwa kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Stade Malien nchini Mali.
Kupitia msemaji wake, Ahmed Ally, Wekundu wa Msimbazi wametoa ujumbe mzito wa hamasa kwa mashabiki na wachezaji, wakisisitiza kuwa bado wana nafasi ya kurekebisha mambo na kuendelea kupambana katika Kundi lao.
Ahmed ameeleza kuwa Simba iko katika wakati wa kuinuka na kuangalia mbele akisema: “Simba muda wa kuinuka na kuangalia mbele. Nafasi bado tunayo, tunyanyuke tuendeleze mapambano.”
Simba inahitaji kurejea kwenye ushindani haraka ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele zaidi, ambapo mchezo wao ujao dhidi ya Stade Malien unatarajiwa kuwa kipimo kingine muhimu cha kuonesha ubora na kurejesha morali ya mashabiki.
Simba licha ya kupoteza mchezo wa kwanza, bado michezo mitano imebaki, jambo linaloipa Simba nafasi ya kurejea vizuri endapo itaweka umakini, nidhamu na mkakati sahihi katika mechi zijazo.
Mchezo dhidi ya Stade Malien unatarajiwa kuwa mgumu, hasa ukizingatia ubora wa wapinzani hao wanapocheza nyumbani, lakini Simba ina rekodi nzuri ya kupambana katika ardhi ya ugenini ndani ya michuano ya CAF.
The post Simba haijakata tamaa yajipanga kurejea kwa kasi first appeared on SpotiLEO.


