YANGA imetibua rekodi nzito ya FAR Rabat iliyoondoka vichwa chini, lakini maumivu makubwa anayo kocha wa timu hiyo, Alexandre Santos aliyeweka wazi anaondoka na jina la kiungo Pacome Zouzoua, aliyekiri ni mchezaji tishio huku akiulizia kuhusu mkataba alionao Jangwani.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Santos amesema Far Rabat imefungwa na Yanga kutokana na Pacome, aliyekiri wachezaji wa timu hiyo ya Morocco kushindwa kumdhibiti kiasi kwa muda mrefu kutumika kuwarudisha wenyeji mchezoni.
Santos amesema, Pacome ni kiungo hatari akiwa na mpira na kwamba ana uamuzi wa kijasiri mkubwa wa kuufungua ukuta wowote kutokana na ujuzi na ubunifu mpira ukiwa miguuni kwake.
“Yanga wana wachezaji wengi wazuri lakini yule namba 10 (Pacome) ni mchezaji hatari zaidi, wakati tunatafuta ubora wa wachezaji wao tuliona makali yake lakini alichokifanya ni zaidi ya kile ambacho tulikiona kabla,” amesema Santos na kuongeza;
“Ana ubunifu sana mpira ukiwa kwenye miguu yake, kuna wakati timu yake ilienda chini lakini akairudisha mchezoni, ni mchezaji mwenye kiwango kikubwa sana, nimeona hata viongozi wanatafuta muda wa mkataba wake.
“Baada ya kumuona kipindi cha kwanza, tukajipanga kumtuliza kipindi cha pili, lakini bado alifungua sana ukuta wetu, nadhani hali ya hewa nayo iliwasumbua wachezaji wangu.”
Santos aliyekuja Tanzania kwa mara ya pili na kupoteza mechi mbili za Bara na Zanzibar, baada ya awali kuja CS Sfaxien ya Tunisia na kulala 2-1 kabla ya juzi kulazwa na Yanga, amesema hatua hiyo imempa maumivu makubwa.
“Nilipokuja hapa mara ya kwanza nilipoteza na Simba (2-1) wakati nikiwa na Sfaxien, lakini nilitaka kubadili kile kilichotokea bahati mbaya tumepoteza na mchezo huu pia hatukutaka kupoteza mchezo wa kwanza,” amesema Santos na kuongeza;
“Mechi hii imeisha kuna mambo yametufundisha tunatakiwa kubadilika haraka kuangalia mchezo utakaokuja ambao tutacheza nyumbani, tunatakiwa kwenda kubadilisha matokeo na haitakuwa rahisi.”
Kama ulikuwa hufahamu Far Rabat mara ya mwisho kupoteza ndani ya dakika 90 ilikuwa Mei 3 mwaka huu ilipocharazwa 2-1 ugenini dhidi ya Wydad Athletic kwenye Ligi ya Morocco na kipigo ch Yanga kimeifanya isitishe safari ya kutofungwa mechi 19 za mashindano yote.
MIPANGO ILIFELI
Far Rabat inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Morocco maarufu Botola Pro 1, hadi sasa imefunga jumla ya mabao 22 na yenyewe kufungwa manne likiwamo la Dube na Santos anasisitiza;
“Tulimaliza kipindi cha kwanza kwa sare ya 0-0 na tuliendelea kupambana. Tuliendelea kwa kufanya baadhi ya mabadiliko, tukabadilisha baadhi ya wachezaji. Tulibadilisha mambo kadhaa ili kupata udhibiti zaidi wa mpira, kumiliki mpira zaidi. Nadhani tulifanikiwa. Tulianza kipindi cha pili kwa matumaini kidogo zaidi, tukiwa na mpangilio wa kina zaidi wa aina yetu ya uchezaji.
“Lakini Yanga walikuwa imara pia. Nakumbuka hili ni bao la nne msimu huu tunaruhusu, na lilikuwa zuri sana. Tulijaribu mara nyingi kudhibiti mchezo,” amesema Santos na kuongeza;
“Lakini tumepoteza mechi ya kwanza ya msimu huu. Inaumiza. Kama nilivyosema, ilikuwa mechi ya ushindani mkubwa, ngumu sana, na tunapaswa kuinuka tena, kuelekeza macho yetu kwenye mechi inayofuata. Tutajiandaa kwa mechi ijayo na kuusahau haraka huu mchezo.
“Hii ndiyo njia yetu, lazima tukubali matokeo. Tunasikitika sana. Mashabiki wetu pia, bila shaka wamesikitika kwa sababu walikuja kutuunga mkono na hawakutaka kuona tukipoteza.”
Baada ya kupoteza mbele ya Yanga, timu hiyo inarudi nyumbani kuipokea Al Ahly Ijumaa hii siku ambayo Yanga itakuwa ugenini kuumana na JS Kabylie ya Algeria iliyoanza makundi kwa kupoteza 4-1 jijini Cairo.
The post PAMOJA NA KUFUNGWA JUZI….WAARABU WABEBA JINA LA PACOME YANGA…. appeared first on Soka La Bongo.


